Dkt. Gwajima Apiga Marufuku Mila na Tamaduni za Vigoma na Vigodoro Tanga

0


Na Saidi Saidi – WMJJWM, Tanga

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amekemea vikali tabia pamoja na mila na desturi zinazofanywa na baadhi ya jamii ambazo zinakiuka maadili na kusababisha mmomonyoko wa maadili katika jamii, hususan kwa watoto. Amewataka wananchi kuacha mara moja vitendo hivyo.

Dkt. Gwajima amesema hayo tarehe 23 Februari 2026, akizungumza na wananchi wa Kata ya Mnyuzi wilayani Korogwe, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea miradi inayotekelezwa na Shirika la World Vision Tanzania kwa kushirikiana na Serikali mkoani Tanga.

Katika mkutano huo, Dkt. Gwajima ameendesha mjadala uliowahusisha wananchi na viongozi wa eneo hilo, kujadili na kutoa maoni kuhusu mila na tamaduni zijulikanazo kama vigoma na vigodoro, ambazo hufanyika hadharani nyakati za mchana. Wananchi wengi wameonesha kukerwa na vitendo hivyo, wakisema vinaathiri maadili ya jamii na kuchochea tabia zisizofaa kwa watoto, hali iliyopelekea azimio la pamoja la kukomesha vitendo hivyo.

Aidha, katika hatua nyingine, Dkt. Gwajima ameongoza maandamano ya akina mama na wanawake wa kata hiyo kupinga vitendo hivyo, akiwataka wanawake kuwa mstari wa mbele katika kukemea mila na desturi zinazoathiri maadili, kwa kushirikiana na wanaume pamoja na Serikali.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, William Simon Mwakilema, amesema kuwa kuanzia tarehe 23 Februari 2026, Serikali kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya itahakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa kabisa ili kulinda maadili ya jamii, hususan kwa kizazi cha sasa na kijacho.

✍️maendeleo ya jamii








Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top