Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ameipa Bodi ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) muda wa miaka mitatu kuhakikisha hakuna Mtanzania anayelazimika kwenda nje ya nchi kupata matibabu ya saratani.
Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Januari 5, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Bodi ya ORCI.
Amesema kuwa Tanzania, chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma za matibabu ya saratani na sasa ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zinazotoa huduma za kisasa katika eneo hilo.
“Ni lazima tuende sambamba na kasi ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za afya, hususan matibabu ya saratani,” amesema Mhe. Mchengerwa.
Kabla ya uzinduzi huo, Waziri Mchengerwa alikagua miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na ORCI, ikiwemo ufungaji wa mashine tatu mpya za tiba ya mionzi aina ya LINAC na Cobalt, upatikanaji wa mashine za kisasa za uchunguzi na matibabu ikiwemo PET CT, pamoja na uanzishaji wa kinu cha kuzalisha dawa za nyuklia (Cyclotron) kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya saratani.
Aidha, Waziri amekagua ujenzi wa jengo jipya la huduma za kimataifa linalolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa ndani na nje ya nchi, huku akiipongeza Menejimenti ya ORCI kwa kutekeleza maelekezo aliyoyatoa Desemba, 2025 ya kufunga na kuanza matumizi ya mashine tatu za uchunguzi wa PET.
Katika ziara hiyo, Waziri Mchengerwa alizungumza na wagonjwa waliokuwa wakipatiwa huduma, ambapo kwa niaba yao Bi. Justina Allen alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha huduma za tiba ya mionzi na kusema kuwa kwa sasa wagonjwa wasio na uwezo wanapata matibabu bure baada ya kufuata taratibu zilizowekwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dkt. Diwani Msemo, amesema kukamilika kwa ufungaji wa mashine hizo mpya kutapunguza muda wa kusubiri huduma kutoka wiki 20 hadi takribani wiki mbili, huku idadi ya wagonjwa wanaohudumiwa kwa siku ikitarajiwa kuongezeka kutoka wagonjwa 200 hadi zaidi ya 400.
Hata hivyo, Waziri Mchengerwa amesisitiza kuwa mageuzi ya huduma za saratani hayapaswi kuishia kwenye majengo au vifaa pekee, bali yajikite pia katika kuboresha mfumo wa utoaji huduma kwa mgonjwa na uzoefu wake wa matibabu kwa ujumla.
Ameiagiza ORCI kuwa wabunifu, jasiri na kuvunja mifumo ya zamani ili kujiimarisha kama kituo cha ubora wa matibabu ya saratani barani Afrika.
Sambamba na hilo, Waziri amesisitiza matumizi ya teknolojia za kisasa, mifumo ya kielektroniki ya taarifa za wagonjwa, usimamizi thabiti wa Bodi, pamoja na kuimarisha utafiti na ushirikiano wa kitaifa na kimataifa ili kuifanya ORCI kuwa taasisi inayoongoza katika matibabu na utafiti wa saratani.
Chanzo : wizara ya afya



.jpg)

.jpg)

