Na Angela Sebastian
Bukoba : Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi(UVCCM) Mkoa wa Kagera Faris Buruhan amewashauri wananchi wa Kata ya Rubale jimbo la Bukoba Vijijini Mkoani Kagera kuendelea kushirikiana kwa karibu na Diwani wao pamoja na viongozi wengine wa Serikali ili kusukuma mbele maendeleo ya kata hiyo, hususan katika sekta za miundombinu, elimu, afya na huduma za kijamii.
Buruhan ameungana na wananchi wa Kata hiyo katika sherehe ya shukrani iliyoandaliwa na diwani wa kata Rubale Julius Rweyemamu ambapo hafla imelenga kuwashukuru wananchi kwaushirikiano wao na kumuunga mkono katika kutekeleza majukumu ya uongozi katika Kipindi cha Miaka mitano ijayo.
Akizungumza katika Sherehe hiyo, Buruhan amewapongeza wananchi wa Tarafa Rubale kwa mshikamano wao, amani na ushiriki mkubwa katika shughuli za kisiasa na kijamii.
Aidha, amewapongeza wajumbe wa CCM wa Tarafa Katerero kumuunga mkono kwa kumpigia kura nyingi katika kura za maoni katika kuwania ubunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini, akielezakuwa matokeo hayo ni ishara ya imani kubwa waliyonayo wananchi kwake hivyo kama Mwenyekiti wa Uvccm mkoa huu wataendelea kushirikiana nao katika kujiletea maendeleo hususani vijana.
“Ushiriki wenu ni mkubwa na kura mlizopiga zinaonyesha imani, mshikamano na ukomavu wa kisiasa, wajibu wetu sasa kuendelea kuwatumikia wananchi kwa bidii na uadilifu, kwa kushirikiana na viongozi walioko madarakani ” amesema Buruhan
Naye Diwani wa Kata ya Rubale Julius Rweyemamu amewashukuru wananchi kwakumuunga mkono na kuahidi kuendelea kusimamia kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wakazi wote wa kata hiyo.
Sherehe hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa chama, serikali pamoja na makundi mbalimbali ya wananchi, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mshikamano na kuhamasisha maendeleo endelevu katika Kata ya Rubale.










