Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya amemtaka Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Tabora kuhakikisha wananchi waliokamilisha taratibu za kumilikishwa ardhi wanapatiwa hatimiliki.
Mhe. Kaspar Mmuya ametoa agizo hilo Januari 10, 2026 mkoani Tabora katika ziara yake ya kikazi mkoani humo wakati wa kikao chake na watumishi wa sekta ya Ardhi kikiwa na lengo la kuwakumbusha utekelezaji wa majukumu yao kikamilifu kwa kuzingatia maadili ya kazi katika utumishi wa umma.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mhe. Kaspar Mmuya ameonesha kutoridhishwa na mwenendo wa utoaji hatimiliki za ardhi kwa wananchi licha ya kukamilisha taratibu zote za kumilikishwa ardhi.
"Kupata hati ya kiwanja iwe kama kutafuta tanzanite au dhahabu nchi hii? Yaani mtu ambaye amekuja kuomba hati amefuata taratibu na kutimiza vigezo vyote vinavyotakiwa inakuwaje inamchukua miaka miwili kupata hati yake?" amehoji Mhe. Mmuya.
Kwa upande mwingine, Naibu Waziri huyo amewataka watumishi wa sekta ya Ardhi nchini kutambulika kama kioo cha haki kwa wananchi kwenye kada zote za sekta ya ardhi.
"Watumishi wote wa Ardhi Tanzania tutambulike kimaadili, kila tukisema na kujitambulisha mimi nafanya kazi wizara ya Ardhi tujulikane na wananchi bila kupepesa macho kuwa huyu ndiye mtetezi wa haki wa wananchi kwenye ardhi" ameongeza Mhe. Kaspar Mmuya.
Naye Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Tabora Bw.Tumaini Gwakisa amewahimiza watalaamu wa Ardhi kutoka wilaya za mkoa wake kutumia fursa ya kuendesha Kliniki za Ardhi katika maeneo yao katika kushughulikia malalamiko ya wananchi.
"Baadhi ya halmashauri ambazo sisi kama Mkoa hatujafika mnaweza kuanza au kuendelea na zoezi la Kliniki ya Ardhi kama njia ya kupunguza malalamiko yasiyo na ulazima" amesema Bw. Tumaini Gwakisa.
Ziara hiyo ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ni mwendelezo wa kukagua, kujifunza na kuhimiza utendaji kazi kwa misingi ya utumishi wa umma kwa watumishi wa sekta ya ardhi ili kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia utu na weledi wa taaluma zao.
Chanzo wizara ya ardhi


