Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb), amesema kuwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imekamilisha taratibu za kumpata mkandarasi kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika Shamba la Bugwema, mkoani Mara ikiwemo mifumo ya usambazaji maji mashambani, hatua itakayowezesha matumizi bora ya rasilimali maji na kuimarisha uzalishaji wa kilimo.
Amesema hayo tarehe 9 Januari 2026 akiwa katika ziara ya ukaguzi wa mradi huo na kueleza kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu hiyo, eneo hilo lenye hekta 3,000 litatumika kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji kwa kufuata taratibu na miongozo iliyowekwa, hali itakayowezesha wakulima kuongeza misimu ya uzalishaji wa mazao kulingana na aina ya mazao yatakayolimwa.
“Msiwe na wasiwasi. Baada ya kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji, shamba hili litakuwa tayari kwa wananchi, ambao watapangwa na kunufaika kwa kulima mara mbili, mara tatu au hata mara nne kwa mwaka kulingana na aina ya mazao watakayochagua,” amesema Mhe. Silinde.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Kanali Evans Ntambi, amesema mkoa huo katika msimu wa kilimo wa mwaka 2025/2026, mkoa umepanga kulima hekta 515,848 na kuzalisha tani 1,211,836, huku msimu wa 2024/2025 mkoa ulilima hekta 512,126 na kuvuna tani 1,208,264.
Mkoa wa Mara una jumla ya hekta 47,899 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji pamoja na skimu 46 za umwagiliaji, zikiwemo skimu zinazoendelea kufanyiwa maboresho ya kiufundi.
Katika hatua nyingine, Serikali imeelekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na Bodi ya Pamba kuratibu shughuli za wakulima kwa kuwapanga katika maeneo yaliyopo na kuwalimia kwa gharama nafuu ili kuhakikisha uzalishaji wa mazao unaendelea kwa msimu husika.
Chanzo: wizara ya kilimo


