Wananchi wa Kata ya Mwang’halanga, Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza tayari wameanza kunufaika na ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mahiga unaotekelezwa na Serikali kwa gharama ya Shilingi Bilioni 4.98, kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua mradi huo Januari 10, 2026, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde amesema, “nimezungukia miradi mingi lakini mradi wa Mahiga uliopo Wilayani Kwimba mkandarasi wake amekuwa mfano mzuri kwa wakandarasi wazawa katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya umwagiliaji nchini.”
Ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo unatokana na maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amesisitiza wakulima waache kutegemea kilimo cha msimu kinachotegemea mvua pekee, na badala yake kujikita katika kilimo cha umwagiliaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Mhe. Ng’walabuza Ludigija ameipongeza Wizara ya Kilimo kwa juhudi kubwa inazozifanya katika kuhakikisha wakulima wanapata fursa ya kulima kwa tija na kuinua uchumi wao.
Amebainisha kuwa Wilaya ya Kwimba ina jumla ya skimu nne za umwagiliaji - Mahiga, Shilanona, Kimiza na Luhala, ambazo zote zimefanyiwa ukarabati na kuongezewa maeneo ya umwagiliaji ili kuwawezesha wakulima kuendesha shughuli za kilimo kwa misimu miwili, yaani msimu wa mvua na kiangazi.
Naye Mhandisi Umwagiliaji wa Mkoa wa Mwanza amesema mradi huo umejumuisha ujenzi wa miundombinu muhimu ikiwemo mifereji mikuu miwili yenye urefu wa jumla ya mita 5,500, mifereji ya shambani, barabara za mashambani zenye urefu wa mita 5,000, vigawa maji na birika la kunyweshea mifugo.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima wa Kata ya Mwang’halanga, Renatus Mauma amesema, “Ni mambo mengi tumepata kupitia mradi huu. Tayari tunavuna na kuendelea na kilimo bila kujali ni masika au kiangazi. Tunaishukuru Serikali kwa kutuletea mradi huu ambao umeboresha maisha yetu.”
chanzo wizara ya kilimo


