▪️Wizara ya Madini na CRDB waingia makubaliano ya utekelezaji wa programu
▪️Wachimbaji wadogo kukopeshwa Mitambo ya Uchenjuaji (CIP), Vifaa vya Kuchimba na Fedha za Uendeshaji
▪️Kikundi cha SAZA GOLD FAMILY wakaribia kuanza kunufaika kupitia leseni ya uchimbaji iliyokuwa inamilikiwa na BAFEX
▪️Ni leseni aliyoelekeza Rais Samia kwa wachimbaji wadogo
Dodoma
Ikiwa ni mkakati wa kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini kimitaji, Wizara ya Madini imeingia makubaliano na Benki ya CRDB kupitia programu maalum kwa ajili ya kuwasadia wachimbaji wadogo kwa kuwapatia mikopo kwa ajili ya ununuzi wa mitambo ya uchenjuaji (CIP), vifaa na gharama za uendeshaji.
Akizungumza kwenye kikao cha kujadili mapendekezo ya ushirikiano kati ya Benki ya CRDB na Tume ya Madini katika utoaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo wa madini, Waziri Mavunde amesema kupitia makubaliano haya, wachimbaji wadogo wenye leseni za madini wataweza kuomba na kupatiwa mikopo na benki hiyo na kuwezesha uzalishaji wao kuwa wenye tija na mchango wao kuendelea kukua kwenye makusanyo ya maduhuli ya Serikali.
Akielezea moja ya wanufaika wa programu hiyo Waziri Mavunde amesema kuwa ni pamoja na kikundi cha SAZA GOLD FAMILY ambapo Benki ya CRDB ipo mbioni kutoa mkopo wa shilingi bilioni 30 kwa ajili ya ununuzi wa mtambo wa kuchenjua madini ya dhahabu na vifaa vya uchimbaji kwa kikundi hicho kinachoendesha shughuli zake katika eneo la Saza mkoani Songwe.
Ameendelea kusema kuwa awali, kupitia ziara ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu katika eneo la Saza, kikundi cha wachimbaji wadogo kupitia Mbunge wa Songwe, Mhe. Philipo Mulugo waliomba kupatiwa leseni ya uchimbaji wa madini, ambapo Rais Samia alielekeza kikundi hicho kupatiwa leseni ya uchimbaji iliyokuwa inamilikiwa na Kampuni ya BAFEX.
Amesema ikiwa ni mkakati wa kuendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini kikundi cha SAZA GOLD FAMILY kilipewa leseni na kuanza kuchimba madini na kuomba mkopo kwa ajili ya mtambo wa uchenjuaji wa madini na vifaa ambapo mchakato wake ulianza mara moja kupitia Benki ya CRDB.
chanzo: wizara ya madini







