👉 Mfumo
wa kifamilia na maamuzi ya kijamii unaendelea kuwaweka wanawake pembeni katika
uwekezaji wa kilimo chenye tija
👉 Ukosefu
wa hati za ardhi na masharti magumu ya mikopo unawazuia wanawake kufikia
teknolojia za umwagiliaji wa solar
👉 Licha
ya sera na bajeti kuongezeka, wanawake wa vijijini bado wako nje ya mapinduzi
ya nishati ya jua katika kilimo
Na
Emmanuel Chibasa
CHAGUA Viongozi Bora Kwa Maendeleo ya
Kilimo, Mifugo Na Uvuvi - Hii ilikuwa kauli mbiu ya serikali
katika maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi (Nanenane) mwaka 2025. Kauli
iliyobeba matumaini ya mageuzi ya kilimo, tija, matumizi ya teknolojia na
ustawi wa wakulima wadogo. Lakini kwa wanawake wengi vijijini, kauli hii bado
inaonekana kuwa ahadi iliyo mbali na uhalisia wa maisha yao ya kila siku.
Wakati wa
sherehe za ufunguzi wa maonesho hayo zilizofanyika kitaifa katika viwanja vya
Nzuguni mkoani Dodoma, Makamu wa Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango alitoa rai kwa viongozi kutambua wajibu wa
kutekeleza Dira ya Taifa 2050 na mipango ya maendeleo ya sekta ya kilimo ambayo
imedhamiria kuongeza kasi ya ukuaji wa kilimo hadi kufikia asilimia 10 kwa
mwaka, ifikapo 2030 na kuendelea.
Alisema viongozi wanapaswa kusimamia uwezeshaji wa wakulima,
wafugaji na wavuvi kiuchumi, hususani upatikanaji wa mitaji, teknolojia, elimu
na mafunzo, pamoja na upatikanaji wa huduma za ugani, ikiwemo kukuza matumizi ya
kanuni bora za kilimo, halikadhalika kuhamasisha maendeleo ya ushirika na
ushirikiano kati ya wakulima,wafugaji,wavuvi na watafiti, maafisa ugani na
watunga sera lakini fursa hizo bado zinaonekana kutowafikiwa baadhi ya wakulima hasa katika maeneo ya
vijijini
Katika kijiji cha Rusoli, Musoma vijijini
mkoani Mara wakulima wanaeleza
kutofikiwa na fursa hizo huku athari za mabadiliko ya tabia nchi zinaonekana
kuwakabili kila msimu kwa hali ukame huku wanawake na watoto wakitajwa kama
kundi linalo athirika zaidi kutokana na kuendesha shughuli za kilimo
kinachotegemea mvua hali inayowaweka katika hatari ya usalama wa chakula na
umasikini wakati ambao Sera na mipango ya taifa inasisitiza kilimo cha
umwagiliaji na matumizi ya nishati jadidifu kama sola lakini kwa wakulima husani wanawake wengi katika kijiji
hicho bado hali ni tofauti kabisa.
Kijiji cha Rusoli kinachokadiliwa
kuwa na wakazi 8,940 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi 2022, sehemu kubwa
ya ardhi inaonyesha kumilikiwa na wanaume huku wanawake wakibaki kuwa watumiaji
wa mashamba ya urithi bila haki ya maamuzi wala umiliki. Mila na desturi
kandamizi na zilizopitwa na wakati, kutokidhi vigezo vya mikopo na uelewa mdogo wa
haki za kisheria vinaendelea kuwazuia wanawake kumiliki na kuwa na maamuzi
katika ardhi pamoja na kufikia mitaji ya kuwekeza katika kilimo cha kisasa.
Licha ya Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 iliyoboreshwa mwaka 2023
kutamka wazi usawa wa kijinsia katika umiliki na urithi wa ardhi, utekelezaji
wake bado haujawanufaisha wanawake katika ngazi ya jamii.
Ripoti za Landesa zinaonesha kuwa
kabla ya mageuzi haya, haki ya mwanamke kurithi ardhi ilikuwa imefungwa na mila
za koo. Ingawa sera mpya imeondoa vikwazo hivyo kisheria, wanawake wengi
vijijini bado wanaishi chini ya maamuzi ya kifamilia na kimila yanayowanyima
haki hiyo kwa vitendo.
Ukosefu wa umiliki wa ardhi
unamaanisha kukosa dhamana kwa wanawake, upelekea kukosa sifa ya kupata mikopo
ya kilimo na hata ufugaji. Taasisi nyingi za fedha bado zinahitaji hati miliki
kama kigezo kikuu cha mkopo. Matokeo yake wanawake hushindwa kununua pampu za
umwagiliaji za sola, mashine za kukausha mazao au teknolojia nyingine
zinazoweza kuongeza tija na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Ni saa nne na dakika ishirini
asubuhi nifika katika kijiji cha Rusoli umbali kilometa 57 kutoka Musoma mjini
nakutana na Bahati Mjarifu Kayema (62),
mama wa watoto sita ambaye pia ni mkulima. Kwa muda niliofika mwanamke huyu
badala ya kuwa shambani, lakini nimemkuta akiwa nyumbani anamenya mihogo kwa
ajili ya kukaushwa ili baadae aweze kusaga na kupata unga kwa ajili ya chakula
cha familia huku akieleza hali ya ukame ndio imemlazimisha kuwa nyumbani kutokana
na ukosefu wa mvua kijijini hapo.
Bahati anasema katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi mwezi Decemba, 2025 mvua imenyesha mara mbili pekee hali iliyopelekea Mahindi na mtama wake kuharibika lakini amefanikiwa kuvuna mihogo na hivyo kupoteza matumaini kabisa ya mavuno ya mazao hayo ambayo yameharibika kutokana na hali ya ukame.
Amesema kwa zaidi ya miaka 20 amekuwa akiendesha shughili za kilimo kwenye ardhi ya urithi ya wazazi wa mume wake bila mafanikio ambapo pia mbali na changamoto ya ukame lakini pia hajawahi kufikiwa na maafisa ugani, taasisi za fedha, wataalamu wa ardhi, wataalamu wa nishati ya umeme jua kwa ajili ya kupewa elimu ya kilimo cha umwagiliaji pamoja na fursa za mikopo ili kukabiliana na hali ya ukame pamoja na elimu ya haki ya kumiliki ardhi.
“Natamani kulima kilimo cha umwagiliaji
Lakini huku maamuzi ya shughuli za kilimo yanatolewa na wanaume, Mashamba ni ya
wanaume ambayo wamerithi kutoka kwa wazazi wao, hata kule nyumbani kwetu
mashamba ya wazazi wetu wanaoyasimia ni wanawame na sina shamba huko sababu tayari
nimeolewa huku.
Natamani
sana kupata mkopo na mbegu bora lakini kama unavyojua bila dhamana mikopo hatupati,
Mvua ndio kama hivi unavyoona mashamba yetu mazao yanaharika njaa inaongezeka na hatujui tutakuwa wageni wa
nani kwa kweli kama serikali inatusikia waje waone hali tuliyonayo ili
watusaidie” Anasema Bahati.
Simulizi ya hii ya Bahati pia
nimeikuta kwa Milka Maregesi
mama wa watoto tisa kutoka kijiji cha Rusoli, anasema pia shamba lake la
mahindi zaidi ya hekari moja limeharibika kwa ukame katika shamba ambalo
linamilikiwa na familia ya mume wake.
“Tunalima kwa kutegemea mvua lakini mazao yetu huwa yameharibika kutokana na ukame, Kule chini kuna shamba lingiine lipo jirani na mto lakini tunatumia maji hayo kumwagilia kwa mikono shamba la mbogamboga. Tunaiomba Serikali itusaidie hata vifaa vya umwagiliaji ili mazao yetu yasiwe yanaharibika” Anasema Milka
Wanawake hawa wanaonekana kuwa waathirika wa moja kwa moja wa mifumo
isiyo rafiki kutokana na mila na desturi, mfumo dume wa umiliki wa ardhi,
vigezo vya kupata mikopo, ukosefu wa elimu ya haki ya kumiliki aradhi na
matumizi ya nishati ya jua katika kilimo wakati ambao serikali kupitia wizara
ya kilimo ikiongeza bajeti ya wizara hiyo kutoka shilingi Bilioni 169.2 kwa
mwaka wa fedha 2021/2022 hadi shilingi Trilioni 1.243 katika mwaka wa fedha
2025/2026.
Buseri
Kubwera ni mwenyekiti wa kijiji cha Rusoli
akizungumza na Musoma Tv amekiri uwepo wa changamoto hizo na kueleza kuwa,
ukame umetokana na wananchi kukata miti hovyo huku pia akieleza wanawake kukosa
maamuzi katika matumizi ya ardhi kwa sababu ardhi inamilikiwa kifamilia na
kurithiwa na wanaume pamoja na kukosekana kwa hati za kimila kwa mashamba
zinachangatia wakulima kushindwa kulima kilimo chenye tija na kutoa fursa kwa
wanawake.
“Kuhusu
swala la mikopo wananchi wengi wameishakata tamaa,unakuta wanaambiwa waunde
vikundi ili waweze kupata mikopo lakini wanapofuatilia wanazungushwa na
kuambiwa hawajitimiza vigezo na hata hiyo mikopo inayotolewa na halmshauri nayo
wananchi wa Rusoli wameishaikatia tamaa.
Changamoto
nyingine ni upatikanaji wa mbegu za ruzuku, huku kwetu hakuna mkulima hata
mmoja aliyefikiwa na hizo mbegu, wakulima wenyewe wanapambana kununua mbegu
madukani tunaiomba serikali iweze
kutuletea na sisi hizo mbegu.
Pia tunaomba serikali na benki kuangalia namna mbadala ya masharti ya mikopo ili yaweze kuendana na hali halisi ya wananchi wa vijijini pamoja na kuwa wanatuambia kuna mikopo lakini masharti yanakua ni magumu ukilinganisha na hali halisi ya wakulima, wafugaji na wavuvi katika kijiji chetu. Ameongeza Majinge
Sheria na Sera kuhusu Umiliki wa Ardhi na Kilimo kwa Wanawake
Haki na
umiliki pamoja na usimamizi wa ardhi nchini Tanzania bado inaonekana kuendelea
kutawaliwa na wanaume ikilinganishwa na wanawake.
Kwa mujibu wa Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC) licha ya
sera mpya ya ardhi kutoa matumaini, sheria za urithi bado hazijarekebishwa
kikamilifu, utekelezaji wa haki ni dhaifu, na wanawake wengi hawajui haki zao.
Fulgence Massawe ni Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) anasema changamoto za kijinsia katika umiliki wa ardhi na upatikanaji wa rasilimali za uzalishaji bado ni kikwazo kikubwa kwa wanawake wengi nchini Tanzania hususan katika maeneo ya vijijini.
Amesema mila na desturi kandamizi zinaendelea kuwapa wanaume mamlaka makubwa ya kurithi na kumiliki ardhi hali inayowanyima wanawake haki ya umiliki au urithi. Katika jamii nyingi ardhi husajiliwa kwa jina la mwanaume pekee jambo linalosababisha wajane wengi kupoteza makazi na mashamba yao baada ya kufiwa, licha ya kuwa wameyatumia kwa miaka mingi.
Ameongeza kuwa ukosefu wa hati na nyaraka za umiliki wa ardhi ni changamoto nyingine inayowakumba wanawake. Wengi wao hushindwa kupata hati za ardhi kutokana na umaskini, uelewa mdogo wa taratibu za kisheria, au kutoshirikishwa katika maamuzi ya kifamilia. Hali hii inawafanya wanawake kukosa usalama wa umiliki na kuwanyima fursa ya kutumia ardhi kama dhamana ya kupata mikopo au uwekezaji wa maendeleo ya kilimo.
Aidha amesema, ucheleweshaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji umeendelea kuongeza hatari kwa wanawake. Takwimu zinaonyesha kuwa ni takribani asilimia 34 tu ya vijiji nchini vilivyokamilisha mipango ya matumizi ya ardhi (Village Land Use Plans – VLUP), hali inayochelewesha upatikanaji wa Hati za Haki ya Umiliki wa Kimila (CCRO). Kutokuwepo kwa mipango hiyo kunawaweka wanawake katika mazingira ya kunyimwa ardhi bila utaratibu wa kisheria, hasa pale migogoro ya ardhi inapojitokeza.” Amesema wakili Massawe.
“Upungufu wa upatikanaji wa rasilimali za uzalishaji nao umeendelea kuwanyima wanawake fursa za kiuchumi. Wanawake wengi wanakosa zana bora za kilimo, pembejeo, mitaji, teknolojia za kisasa, mafunzo, pamoja na huduma za ugani. Ripoti zinaonyesha kuwa ni asilimia ndogo sana ya wanawake wenye hati rasmi za ardhi, hali inayowagharimu uwezo wa kupata mikopo kutoka taasisi za fedha na kuwekeza katika shughuli za uzalishaji.
Katika hatua za sera, Tanzania
imeanza kufanya mageuzi yanayotoa matumaini. Toleo jipya la Sera ya Taifa ya
Ardhi ya mwaka 2023, lililozinduliwa mwaka 2025, limeondoa baadhi ya vikwazo
vya muda mrefu vilivyokuwa vinaruhusu mila na desturi kuzuia wanawake kurithi
na kumiliki ardhi. Sera hiyo inatamka wazi usawa wa kijinsia katika upatikanaji
wa ardhi na inasisitiza ushiriki wa wanawake katika mifumo ya utawala wa ardhi.” Amesema Massawe
Matokeo utafiti yaliyotolewa na
Social Intitutions and Gender Index (SIGI), November 2021,pia zinaonesha kuwa, wanawake ni asilimia 43.2 ya wamiliki
wa ardhi za kilimo, lakini ni asilimia 17.1 tu wanaomiliki ardhi peke yao, huku
upatikanaji wa huduma rasmi za kifedha ukiwa asilimia 45.8 pekee.
Hali ya Upatikanaji wa Mikopo kwa Wanawake.
Hali ya
upatikanaji wa mikopo kutoka katika taasisi za fedha ikiwa ni pamoja na benki
kwa wanawake kwa ajili ya shughuli za kilimo bado inaonekana kuwa changamoto
kubwa hali inayodaiwa kuchangiwa na uelewa mdogo juu ya fursa zilizopo pamoja
na mifumo iliyopo katika familia inayotokana na mila na desturi zilizopitwa na
wakati.
Sospeter
Justin ni meneja wa NMB Bank tawi la
Musoma, anasema kuwa wanawake wengi wanachangamkia mikopo ya biashara ndogo za
ujasiliamali hasa katika maeneo ya mjini lakini wanabaki nyuma kwenye mikopo ya
kilimo na ufugaji kwa sababu ya kukosa dhamana ya hati za mashamba na nyumba,
taarifa za mapato na matumizi pamoja na kutokua na akaunti kwa ajili ya kuweka
fedha huku akikiri kuwa matatizo hayo kuanzia ngazi ya familia kutoana na vitu
vingi kusimamiwa na wanaume.
"Sisi kwa wateja wanaotaka mikopo, miongoni mwa
mashari ambayo mteja anatakiwa kutimiza ni pamoja na kuwa na hati ya nyumba,
leseni pamoja na TIN Namba pamoja na kuwa na akaunti katika taasisi za kifedha.
Katika
familia nyingi hasa huko vijijini nafikiri bado wanawake hawapewi nafasi
kutumia ardhi iliyopo kwa ajili ya kilimo na ufugaji ndio maana unaona wanaume
ndio wananufaikia zaidi ikilinganishwa na wanawake lakini sisi tunatoa mikopo
kwa makundi yote ilimradi tu watimize vigezo” Amesema Sospeter
Changamoto ya Matumizi ya
Nishati ya Jua kwa Wanawake
Matumizi ya teknolojia za nishati ya
jua katika kilimo cha umwagiliaji, uhifadhi, ukaushaji na usindikaji wa mazao
yana uwezo mkubwa wa kuongeza uzalishaji kwa wakulima wadogo na kupunguza
gharama za kazi kwa wanawake vijijini. Hata hivyo bado kuna pengo kubwa la
ujumuishaji wa kijinsia, kwani teknolojia hizi haziwafikii wanawake kwa kiwango
sawa na wanaume. Sababu kuu ni ukosefu wa fedha, mila na desturi, pamoja na
masharti na vigezo vya kupata mikopo.
Mhandisi Adrian Edwin, mtaalam wa
nishati ya jua kutoka Elico Foundation, anasema wanawake wengi vijijini
wanaendesha kilimo kwenye mashamba ya urithi yanayomilikiwa na wanaume, hali
inayowanyima sifa ya kupata mikopo. Anaeleza kuwa hata pale teknolojia za sola
zinapopatikana, wanaume ndio wanaozichangamkia zaidi huku wanawake wakikosa
sapoti ya kifamilia kutokana na mila zinazomzuia mwanamke kumiliki ardhi.
Anabainisha kuwa licha ya kuwepo kwa sera na sheria zinazotambua haki ya
wanawake kumiliki ardhi, jamii bado inashikilia mtazamo kuwa mwanamke ataolewa
na kuondoka, hivyo kumtenga kwenye maamuzi na fursa za uwekezaji wa nishati ya
jua.
Wanawake wa Rusoli bado wanakabiliwa
na vikwazo katika upatikanaji wa umwagiliaji unaotumia nishati ya jua, lakini
juhudi za kikanda zinaonyesha kuwa suluhisho linawezekana. Kulingana na Ashoka East Africa Newsletter (mei
2025), katika Mkutano wa Ashoka Changemakers uliofanyika April 11, 2025,
Nairobi nchini Kenya sehemu ya mradi wa Mott Foundation “Towards Improving the Livelihood of Smallholder Farmers in East
Africa” wasemaji walionyesha pia mifano ya kazi katika sekta za nishati,
chakula, maji na usimamizi wa taka kuwa ni asilimia 33 tu ya ubunifu wa
tabianchi unasimamiwa na wanawake na kueleza kuwa kuna haja ya haraka ya kuunga
mkono suluhisho jumuishi.
Tafiti zinaonesha kuwa changamoto
hizi zinazidishwa na gharama kubwa za awali za teknolojia za sola na ukosefu wa
mikopo rafiki. Takribani asilimia 90 ya wakulima bara la afrika ambao
wangefaidika na pampu za maji zinazotumia nishati ya jua hawawezi kuzimudu.
Hali hii pia inawaacha wanawake wengi vijijini nje ya mapinduzi ya matumizi ya
nishati ya jua yanayoweza kubadilisha kilimo na maisha yao.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Muongozo wa
Uwekezaji wa Mkoa wa Mara (Mara Investment Guide, 2020), mkoa una takribani
hekta milioni 2.5 za ardhi, ambapo hekta 500,000 zinafaa kwa kilimo. Kati ya
eneo hilo, hekta 3,634.10 sawa na asilimia 7.5 zinafaa kwa kilimo cha
umwagiliaji kutoka vyanzo vya maji vya Ziwa Victoria, mito na mabwawa, huku
Wilaya ya Musoma ikitajwa kuwa miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa za
kuendeleza kilimo cha umwagiliaji.
Hata hivyo hali halisi katika kijiji
cha Rusoli, Musoma vijijini, inaonyesha kuwa wakulima wengi bado wanategemea
mvua licha ya uwepo wa Ziwa Victoria. Wakulima wachache huendesha bustani ndogo
ndogo za mbogamboga kwa kusomba maji kwa mikono kutoka ziwani na mitoni,
kutokana na umaskini unaowazuia kumudu vifaa vya umwagiliaji kama pampu za
nishati ya jua..
Hatua za
Kupunguza Ukosefu wa Usawa wa Kijinsia katika Kilimo na Uwekezaji
Makamu wa Rais wa Chemba ya
Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Boniface Ndengo,
amesema wanawake wanakabiliwa na changamoto nyingi zinazopunguza ushiriki wao
katika uwekezaji na kilimo cha kisasa. Ameeleza kuwa changamoto hizo haziathiri
teknolojia za kilimo pekee, bali sekta zote za uwekezaji, hali inayowafanya
wanawake wengi kubaki katika biashara ndogo ndogo huku fursa kubwa zikiwapita.
Ndengo amesema mfumo wa uwekezaji
unaotegemea dhamana kubwa unawanyima wanawake fursa, kwa kuwa wengi hawana mali
za kuweka dhamana. Matokeo yake, wanawake hulazimika kutegemea mikopo midogo
yenye riba kubwa na kushindwa kuwekeza katika teknolojia za kilimo. Ameongeza
kuwa hali hii inaathiri moja kwa moja familia, kwani wanawake wanapokosa fursa
za kiuchumi, umasikini huendelea katika ngazi ya kaya.
‘TCCIA imefanya maboresho ya sera na
katiba zake ili kuyawezesha makundi maalum yakiwemo wanawake kupata fursa kubwa
za kibiashara katika teknolojia, mitaji na masoko. Amebainisha kuwa ushirikiano
kati ya TCCIA, Serikali na wanachama wake ni muhimu katika kukuza uwekezaji
jumuishi, hususan katika ardhi na kilimo cha umwagiliaji.” Amesema Ndengo
Lipi Jukumu la vyombo vya habari Katika Kuelimisha Jamii
Vyombo vya habari vina jukumu muhimu
katika kuelimisha jamii juu ukosefu wa usawa wa kijinsia katika umiliki wa
ardhi na sekta ya kilimo.
Jovina Masano ni Mwenyekiti wa Chama
cha Waandishi wa Habari Wanawake Wenye Maono Mkoa wa Mara anasema vyombo vya
habari vinajukumu kubwa la kutoa elimu kuhusu mila, desturi na mitazamo ya
kijamii inayowaona wanawake kama watu
watakaoolewa na kuondoka katika ardhi ya asili.
“Vyombo
vya habari vina wajibu wa makusudi wa kuibua masuala ya wanawake kwa utafiti wa
kina hasa kwa kuwafikia wanawake wa vijijini kwa elimu sahihi kuhusu haki zao,
umiliki wa ardhi, mikopo na teknolojia za kilimo. Kupitia simulizi za jamii na
mafunzo kwa wanawake na wasichana waandishi wa habari wanaweza kuchangia
mabadiliko chanya na kupunguza pengo la kijinsia.” Amesema Jovina
Kwa kuimarisha usawa wa kijinsia katika umiliki wa ardhi, upatikanaji wa mitaji, ubunifu na matumizi ya teknolojia za kilimo, wanawake wanaweza kuwa nguzo muhimu ya usalama wa chakula na maendeleo ya uchumi. Hata hivyo bila utekelezaji thabiti wa sera, mabadiliko ya mitazamo ya kijamii na mchango wa vyombo vya habari, pengo la kijinsia litaendelea kuwakosesha wanawake fursa na kuendeleza mzunguko wa umasikini vijijini.





