Haji Mtete Aitaka Kamati ya Maendeleo Kata ya Nyasho Kutekeleza Miradi ya Maendeleo Kwa Ushirikiano

0


Na Ghati Msamba-Musoma

Naibu Meya wa Manispaa ya Musoma, Haji Mtete, amewataka wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) ya Kata ya Nyasho kushirikiana katika kutatua changamoto zinazojitokeza kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ili kuhakikisha kata hiyo inakuwa na mandhari nzuri na yenye kuvutia.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati akifungua kikao cha WDC kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo katika ofisi za Kata ya Nyasho.

Aidha, amewasisitiza wajumbe hao kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha maendeleo ya kata yanapatikana, badala ya kuendeleza majungu yasiyo na tija. Pia ametoa wito wa kuzingatia nidhamu katika utendaji wa kazi na kuheshimiana baina ya viongozi.

Haji amesema kuwa katika kipindi chake cha uongozi, kwa kushirikiana na Diwani wa Viti Maalum, Naima Minga, wamefanya jitihada kubwa kuomba na kusimamia upatikanaji wa fedha za maendeleo, hali iliyochangia kata hiyo kupiga hatua kubwa kimaendeleo.

Ametaja kuwa miongoni mwa miradi iliyotekelezwa ni ujenzi wa Soko la Machinga la Mlango Mmoja, ambalo amesema ni lenye mvuto na manufaa makubwa kwa wafanyabiashara wadogo.

Ameongeza kuwa viongozi wataendelea kusimamia miradi hiyo ili iwe na tija kwa wafanyabiashara, hususan machinga.

“Kata ya Nyasho ni miongoni mwa kata zinazopiga hatua kubwa kimaendeleo, hivyo hatuna budi kushirikiana kwa pamoja na kusimamia miradi kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo iliyotungwa na nchi yetu,” amesema Haji.

Ameeleza kuwa kipaumbele cha madiwani ni kushawishi na kuhakikisha fedha za miradi ya maendeleo zinapatikana kwa ajili ya wananchi.

Akizungumzia mikopo inayotolewa kwa vijana, Haji amesema kata hiyo imefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika upatikanaji wa mikopo hiyo, hasa kwa vijana, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupunguza umaskini katika jamii.

Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalum, Naima Minga, amewataka viongozi na wajumbe wa WDC kufanya kazi kwa mshikamano na kuacha masuala ya uchaguzi kwa kuwa tayari yamepita, akisisitiza kuwa bila ushirikiano wa pamoja maendeleo hayawezi kupatikana.

Aidha, Naima amezungumzia suala la maeneo ya wazi (Open Spaces) yaliyovamiwa, akisema kuwa hawatasita kuwachukulia hatua za kisheria wanaokiuka taratibu. Amewataka wananchi wanaohitaji kutumia maeneo hayo kufuata utaratibu wa kisheria kwa kuwasilisha maombi rasmi badala ya kujimilikisha.

Amewaomba viongozi wa kata na wenyeviti wa mitaa kusimamia suala hilo kikamilifu ili kudumisha mji wa sheria.

Kwa upande wao, wajumbe wa kikao hicho wamewapongeza madiwani hao wawili kwa kuchaguliwa tena kuongoza, na kuwaomba waendelee kuwa mstari wa mbele katika kusimamia shughuli za maendeleo. Pia wameomba suala la kodi liangaliwe upya, wakibainisha kuwa wajasiriamali wadogo kama wauza mboga, nyanya na matunda wanatozwa kodi sawa na wafanyabiashara wakubwa, hali inayowakwaza kiuchumi.

Akizungumzia masuala ya elimu, Mratibu wa Elimu wa Kata ya Nyasho, Stephen Katunzi, ameomba kuundwa kwa tume maalum itakayosaidia kuboresha sekta ya elimu ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi. Amesema Shule ya Msingi Nyasho imeshuka kiwango cha ufaulu na kushika nafasi ya 14 kati ya shule 16 za Halmashauri ya Manispaa ya Musoma.

Katunzi amesema kuwa wamejipanga kuwapima wanafunzi wa Darasa la Pili mwaka huu kupitia mitihani ya kitaifa. Hata hivyo, ametaja changamoto ya uchangiaji wa chakula shuleni kwa ajili ya lishe ya watoto pamoja na uzembe wa baadhi ya walimu kutohudhuria vipindi. Kutokana na hilo, Naibu Meya amemuagiza Mratibu huyo kufuatilia kwa karibu mahudhurio ya walimu shuleni.

Katika kikao hicho, wajumbe pia wameomba kusaidiwa kuwekewa umeme katika jengo la ofisi yao. Diwani wa Viti Maalum, Naima Minga, amesema tayari amezungumza na Mbunge wa Viti Maalum, Agnes Marwa, ambaye ameahidi kuunga mkono juhudi za uwekaji wa umeme katika jengo hilo.


Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top