Halmashauri 16 za mikoa ya Mwanza, Geita, Shinyanga na Simiyu zimepatiwa mgao wa mbolea wa tani 22 kupitia Mradi wa Kuwezesha Upatikanaji wa Pembejeo za Kilimo Tanzania (Tanzania Agricultural Inputs Support Project – TAISP) wa Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kuendeleza mashamba darasa yaliyoanzishwa katika Halmashauri hizo.
Zoezi la ugawaji wa mbolea limefanyija tarehe 22 na 23 Desemba 2025 kwa lengo la kuimarisha vituo vya kujifunzia kwa wakulima katika mashamba darasa ili wapate elimu ya teknolojia sahihi za kilimo, matumizi bora ya pembejeo na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.
Halmashauri zilizopokea mbolea hizo ni pamoja na Sengerema, Magu, Kwimba na Misungwi (Mkoani Mwanza); Kishapu, Shinyanga DC, Kahama Manispaa na Msalala (Mkoani Shinyanga); Bukombe, Mbogwe, Chato na Geita DC (Mkoani Geita); na Halmashauri za Mkoa wa Simiyu ambazo ni Maswa, Bariadi DC, Itilima na Busega.
Jumla ya mashamba darasa 226 yameanzishwa katika Halmashauri hizo na yanatarajiwa kuwanufaisha moja kwa moja wakulima 7,080 katika mikoa husika.
Maafisa Viungo katika Halmashauri zilizopokea mbolea wameeleza kuwa tangu kuanza kwa mradi wa TAISP, wakulima wameonesha ari ya kuzingatia mafunzo wanayopatiwa, hali inayochangia uelewa wa teknolojia sahihi za kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao.
WIzara ya Kilimo kupitia Mradi wa TAISP itaendelea kushirikiana kwa karibu na halmashauri na wadau mbalimbali wa Sekta ya Kilimo katika kuhakikisha kuwa mashamba darasa yanatumika ipasavyo kama vituo vya kujifunzia kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji wa mazao, kipato na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Chanzo: wizara ya kilimo


