Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Mha. Athumani Kilundumya, ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kuhakikisha inatekeleza tafiti zenye ufanisi, weledi na matokeo yanayoonekana kupitia Maabara Kuu ya Kisasa ya Kilimo iliyopo Mtumba, jijini Dodoma.
Mha. Kilundumya ametoa kauli hiyo tarehe 22 Desemba 2025 wakati wa hafla ya kupokea na kukabidhi mradi wa jengo hilo, akisema Wizara ya Kilimo imeridhishwa na ubora wa ujenzi wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 16.76 na kumpongeza mkandarasi kwa kutekeleza mradi huo kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha.
Maabara hiyo inayosimamiwa na Wizara ya Kilimo kupitia TARI, ina maabara 15 za kisasa zenye uwezo wa kufanya uchunguzi wa changamoto mbalimbali katika Sekta ya Kilimo kwa lengo la kuongeza tija na ushindani wa uzalishaji wa mazao nchini. Huduma hizo ni pamoja na uchunguzi wa afya ya udongo, utambuzi wa visumbufu vya mimea, tathmini ya ubora wa mbegu pamoja na uchunguzi wa viini lishe vilivyomo kwenye mazao ya kilimo.
Pia, maabara ina hadhi ya maabara ya rufaa ya kilimo ambapo itajihusisha na upimaji wa vimelea vya sumukuvu na sumukuvu katika mazao, hatua itakayosaidia kulinda afya ya walaji, kuimarisha ubora wa mazao na kuongeza fursa za masoko ya kilimo ndani na nje ya nchi.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Stephen Nindi; Mratibu wa Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu Tanzania (TANIPAC), Bw. Clepin Josephat; Menejimenti ya Wizara ya Kilimo pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).
Chanzo: wizara ya kilimo


