Na. Angela Msimbira, MOROGORO
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Elimu kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Elimu ya Msingi, Bi. Suzan Nussu amesema jumla ya wakuu wa shule na wenyeviti wa kamati za shule 3,202 nchini wanapatiwa mafunzo kuhusu usimamizi wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu kupitia Programu ya Uboreshaji wa Elimu ya Awali na Msingi (BOOST).
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo mkoani Morogoro, Bi. Nussu amesema mafunzo hayo yameandaliwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, yakiwa na lengo la kuwajengea uwezo washiriki katika kusimamia ipasavyo fedha na miradi ya miundombinu ya shule.
Ameeleza kuwa mafunzo hayo yanawalenga viongozi wa shule zilizopokea jumla ya shilingi bilioni 222 katika mwaka wa fedha 2024/2025 chini ya Programu ya BOOST, ambapo washiriki wataelekezwa juu ya matumizi sahihi ya fedha hizo ili kuepusha hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuongeza tija katika utekelezaji wa miradi.
“Wakuu wa shule na wenyeviti wa kamati watajengewa uelewa wa kina kuhusu taratibu za usimamizi wa miradi, ili kuhakikisha fedha zinatumika kama ilivyokusudiwa na matokeo yanaonekana,” amesema Bi. Nussu.
Aidha, amebainisha kuwa katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Mradi wa BOOST, jumla ya shilingi bilioni 311.3 zilipelekwa shuleni kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya 379 za awali na msingi. Kupitia fedha hizo, zilijengwa vyumba vya madarasa 10,462, matundu ya vyoo 16,180, majengo ya utawala 379, mabweni 2, nyumba za walimu 51 na vichomea taka 379, huku shule 46 zikifanyiwa ukarabati.
Bi. Nussu amesisitiza kuwa mafunzo hayo ni hatua muhimu katika kuhakikisha uendelevu na ubora wa miundombinu ya elimu nchini, ili kutoa mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia kwa watoto wa elimu ya awali na msingi.
Chanzo: Tamisemi