Christina Ndengo Aeleza Vipaumbele vyake Akichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini

0


Na Ghati Msamba

Musoma: Mgombea ubunge wa Jimbo la Musoma Mjini kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Christina Ndengo, amewaomba wananchi wa jimbo hilo wamchague katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025 ili aweze kushirikiana na Serikali kufufua viwanda vilivyosimama na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni za chama hicho uliofanyika Septemba 14, 2025 katika eneo la Bweri Senta, Kata ya Bweri, Manispaa ya Musoma, Ndengo alisema kusimama kwa viwanda kumeathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa wananchi wa Musoma na kuwaacha vijana wengi bila ajira.

Alisema iwapo viwanda hivyo vitafufuliwa vitasaidia kuongeza ajira kwa vijana, kukuza uchumi wa wananchi na pia kutoa soko kwa mazao ya wakulima, hususan zao la pamba.

“Kusimama kwa viwanda kumepelekea wakulima kushindwa kulima pamba kwa wingi. Wakulima wanajiuliza, wakilima watauza wapi? Nikichaguliwa, nitasimamia kufufuliwa kwa viwanda ili kuongeza thamani ya mazao na kuimarisha kilimo,” alisema.

Akizungumzia sekta ya elimu, Ndengo aliahidi kuwa kila shule ya sekondari isiyo na maabara katika Manispaa ya Musoma itajengewa maabara ili kuwezesha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi kwa vitendo na kuongeza ufaulu.

Aidha, alisema ataiomba Serikali kuongeza ajira za walimu wa sayansi kutokana na uhaba uliopo unaoathiri matokeo ya wanafunzi. Pia aliahidi kusimamia kwa uwazi na uadilifu Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ili unufaishe walengwa.

Kwa upande wa vijana, Ndengo alisema atahamasisha ubunifu na matumizi ya teknolojia mbalimbali ili kujiletea maendeleo sambamba na mapinduzi ya viwanda.

Alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya uchaguzi akisisitiza kuwa kura ndiyo silaha ya kuleta mabadiliko na kuchagua viongozi sahihi.

“Naomba wananchi wa Musoma waendelee kufanya kazi halali kwa bidii ili kujipatia kipato, huku wakijiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani,” alisema.

Katika mkutano huo, wananchi walieleza matarajio yao ya kupata mbunge atakayesimamia kikamilifu utatuzi wa changamoto zilizopo, ikiwemo ubovu wa barabara katika kata za pembezoni, uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi katika baadhi ya sekondari na utekelezaji wa sera ya matibabu bure kwa wazee wasiojiweza.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top