Serikali Yawashauri Walimu na Jamii Kuimarisha Usalama wa Watoto Shuleni

0



Na Angela Msimbira, Morogoro

Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kutekeleza Mpango wa Shule Salama nchini, ikitoa wito kwa walimu wakuu, wenyeviti wa kamati za shule na jamii kuhakikisha usalama wa watoto unazingatiwa kama kipaumbele cha kwanza katika mazingira ya shule.

Akizungumza wakati wa mafunzo kuhusu mpango huo, Mkufunzi Mkuu wa Chuo cha Ualimu Mpwapwa, Juma Kizija, amesisitiza kuwa usalama wa mtoto shuleni ni wajibu wa pamoja unaohitaji mipango madhubuti na ushirikiano wa karibu kati ya wadau wote wa elimu.

Kizija amewashauri walimu wakuu kuandaa mikakati ya mapema ya kuboresha miundombinu, ikiwemo kuhakikisha madarasa, vyoo, njia za kupitisha wanafunzi na maeneo ya michezo yanakuwa salama, rafiki na yenye kuzingatia utu wa mtoto.

Aidha, amesisitiza kuwa kamati za shule zinapaswa kushirikiana kikamilifu na wazazi na jamii ili kubaini mapema changamoto za kiusalama na kuzitafutia ufumbuzi wa pamoja. “Shule siyo jengo pekee, bali ni kituo cha malezi, ulinzi na ujenzi wa tabia. Kila hatua ya maendeleo lazima izingatie haki na usalama wa mtoto,” amesema

Walimu wakuu pia wamekumbushwa kuwa na mifumo thabiti ya kuripoti matukio ya ukatili, manyanyaso au viashiria vyovyote vya hatari dhidi ya wanafunzi, pamoja na kuwapa watoto elimu ya tahadhari juu ya usalama wao wakiwa shuleni na wanaporudi majumbani.

Kizija ametoa wito wa kuachana na dhana ya kuiachia shule jukumu la malezi, akisema malezi bora hufanikiwa pale ambapo wazazi wanashiriki kikamilifu katika mikutano, maamuzi na shughuli za shule.

Amesisitiza kuwa mafanikio ya elimu hayatafikiwa iwapo watoto hawapo katika mazingira salama. Kujenga kizazi chenye nidhamu, maarifa na matumaini ya baadaye kunahitaji shule zinazolinda utu, usalama na haki za mtoto.

Kupitia ushirikiano wa walimu, wazazi na viongozi wa shule, Mpango wa Shule Salama unaweza kufanikisha mabadiliko chanya na kuchochea mustakabali mwema wa elimu nchini.

Chanzo: Tamisemi





Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top