Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC) kuhakikisha mikataba ya ubia inalenga Dira ya maendeleo 2050.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Kishauri wa PPPC, Bi. Flora Tenga katika hitimisho la mafunzo ya Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, yaliyoratibiwa na kutolewa na PPPC, kuanzia tarehe 7 hadi tarehe 9 Oktoba, 2025 Jijini Dodoma.
Bi Flora Tenga aliwashukuru na kuwakumbusha Mawakili wa Serikali kuzingatia na kuyafanyia kazi mafunzo waliyopokea kwani kupitia mafunzo hayo wataweza kusaidia kuleta maendeleo ya Taifa.
*“Lakini pia niwashukuru sana Mawakili wa Serikali kwa kuonesha kiu ya kutaka kujifunza, sababu dunia ya sasa si ya kivyetu vyetu, tupo katika ubia, kwa hiyo tukiwa na wataalamu ambao kweli wamepikwa, wanaelewa namna gani ya kuweza kutafsiri mikataba lakini pia kui draft ni jambo zuri ambalo litapelekea sisi kama Serikali kutimiza malengo yetu.”* Anasema Bi Flora Tenga
Awali akizungumza katika Mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi Uratibu Bw. Ipyana Mlilo aliushukuru Uongozi wa PPPC, kwa kuratibu na kudhamini mafunzo kwa Mawakili wa Serikali kwani kupitia mafunzo haya watakuwa wabobezi katika kupitia mikataba ya ubia.
*“Kwa niaba ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali nipende kuwashukuru PPPC kwa kuwezesha na kufadhili mafunzo haya, kupitia mafunzo haya Mawakili wanajua sekta ya mikataba ya ubia, na kwa uelewa na ubobezi wataweza kupitia mikataba ya ubia kwa weledi”.* Anasema Bw. Mlilo.
Mafunzo kwa Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuhusu mikataba ya Ubia yamefanyika kuanzia tarehe 7 Oktoba, hadi 9 Oktoba, 2025 Jijini Dodoma.
Chanzo: ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali