📌 Awaasa kuviishi viapo vyao
📌 Awasisitiza kutekeleza majukumu kwa kuzingatia Katiba na Sheria za Nchi
📌 Awataka kuzingatia Kanuni za Kimahakama ikiwemo kutochelewa haki bila sababu za kimsingi
📌 Awasihi kutoendekeza masharti ya kiufundi katika kazi ya utoaji haki
📌 Ahimiza utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi
📌 Awataka pia Mahakama hao waliokuwa na chembechembe za uanaharakati na siasa kuacha mara moja
Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju tarehe 07 Oktoba, 2025 amewaapisha jumla Mahakimu Wakazi wapya 89 na kuwataka kuviishi viapo vyao wanapokeleza majukumu yao.
Hii ni mara ya kwanza kwa Jaji Mkuu, Mhe. Masaju kufanya uapisho wa Mahakimu hao wapya tangu kuapishwa kwake kushika nafasi hiyo miezi mitatu iliyopita.
Akizungumza na Mahakimu hao mara baada ya kuwaapisha kwenye ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Mhe. Masaju amewapongeza Mahakimu hao na kuwataka kuviishi viapo vyao sawasawa na walivyoapa.
“Nina machache sana ya kuwashauri leo, moja karibu kila mmoja aliyekula kiapo hapa alikuwa ameshika Biblia au Quran, hivyo nikaamini kwamba tunatambua uwepo wa Mwenyezi Mungu, ushauri wangu kwenu ni kwamba nendeni mkiishi hicho kiapo sawasawa na jinsi mlivyoapa, ninapenda kuamini kwamba mlipokuwa mnaapa hiki kiapo mlikichukulia kwa dhati basi enendeni mkakiishi hiki kiapo,” amesema Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju amesisitiza kuwa, “Mungu hadhihakiwi, unachokipanda ndicho utakachokivuna, kama ulishika Biblia au Quran ukayatamka yale maneno kuanzia kuwa muaminifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kufanya maamuzi yako kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria za Nchi na mila na desturi za Tanzania na bila upendeleo, chuki, uwoga na huba nendeni mkaishi hicho kiapo hicho ndicho mlichopanda na ndicho mtakachovuna.”
Aidha, Jaji Mkuu amewahakikishia Mahakimu hao kwamba, wao kama Viongozi, Walezi lakini pia kama wazazi wao wanawapa baraka zote kama wataenda kukiishi kiapo hicho kwa kuwa wamepewa heshima kubwa.
“Baada ya uapisho huu, mtaenda kwenye mafunzo elekezi na pale tutawakuta Viongozi wetu wa dini watawashauri na kuwaasa kila mmoja hapa ili mnavyotenda shughuli zenu hizi mjue kwamba mnapaswa kuzitenda, mnasimama badala ya Mwenyezi Mungu hapa duniani na wengi wenu mtaenda kufanya kazi vijijini, mtakuwa watu wa kipekee sana huko vijijini, wataendelea kuwaheshimu na ninyi waheshimuni wale watu wanaokuja mbele yenu muwatendee kwa haki sawasawa na viapo vyenu,” amesema Mhe. Masaju.
Amewasisitiza kutenda haki sawa kwa wote bila kuwasahau wajane, maskini, yatima hivyo wasichukulie kigezo cha unyonge wa makundi hayo kupora haki zao kwa kutumia kalamu zao.
“Anayewaonea watu hao, Mungu atamuadhibu lakini na sisi tuna utaratibu wa kuwajibishana, niwaombeni sana tumekuwa na utaratibu hapa kwamba wanaokiuka maadili ya utumishi wetu, tunawachukulia hatua za kinidhamu kwa utaratibu tunaouweka, kama ukiukwaji wa maadili yetu pia ni kosa la jinai mimi ningependa huyu mtu tumpeleke Mahakamani kwanza na yeye ajifunze badala ya kumsimamisha tu halafu kufanya mchakato wa ushughulikiaji wa nidhamu ambao nao unachukua muda mrefu, kwa hiyo kukiwa na ushahidi wa kutosha, Vyombo vya Dola vinavyohusika na kutekeleza iwe ni Jeshi la Polisi, iwe ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) watachukua hatua ipasavyo hakutakuwa na cha kusema kwamba huyu ni Hakimu au ni nani,” ameeleza Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju ameongeza kwa kurejea kauli iliyotolewa na Hayati Mwalimu Nyerere alipokuwa anahutubia mkutano wa Majaji mwaka 1981 jijini Arusha alisema, “Zipo kazi zinazoweza kufanywa na watu tunaowatilia mashaka lakini Uhakimu na Ujaji sio mojawapo ya kazi hizo, Jaji au Hakimu akitiliwa mashaka hata kama ushahidi hautoshi ni lazima aanze kuchunguzwa mara moja.”
Aidha, Jaji Mkuu amewaeleza Mahakimu hao kuhusu Kanuni zitakazowaongoza katika utumishi wao ambazo zinapatikana kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara 107A, 107B na Ibara ya 26. Ibara ya 107A inasema, ‘Mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni Mahakama.’
“Masuala ya haki mamlaka yenye kauli ya mwisho ni Mahakama, ni kana kwamba tunachukua nafasi ya Mungu hapa duniani hapa Tanzania, ndio maana nawasisitiza kwamba haya mlioapa muende muyaishi, mtakuwa na kauli ya mwisho haijalishi wewe ni Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ambayo ni Mahakama ya ngazi ya chini kabisa katika mfumo wa Mahakama za Tanzania bado utakuwa na hiyo kauli ya mwisho na kama mtu hajaridhika na uamuzi wako atakata rufaa Mahakama ya Wilaya na pengine hadi Mahakama ya Rufaa,” amesema Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu ameongeza akirejea Ibara 107A(2) isemayo, “katika kutoa uamuzi wa mashauri ya madai na jinai kwa kuzingatia sheria, Mahakama zitafuata kanuni zifuatazo: - a) Kutenda haki kwa wote bila kujali hali ya mtu kijamii au kiuchumi b) Kutochelewesha haki bila sababu ya kimsingi c) Kutoa fidia ipasavyo kwa watu wanaoathirika kutokana na makosa ya watu wengine na kwa mujibu wa Sheria mahsusi iliyotungwa na Bunge d) Kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika migogoro na e) Kutenda haki bila kufungwa kupita kiasi na masharti ya kifundi yanayoweza kukwamisha haki kutendeka.
Aidha, amewasihi Mahakimu hayo kutoa ushauri wa kufanya usuluhishi kati ya wadaawa ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha wadaawa faida na hasara za kuendelea au kutoendelea na shauri Mahakamani.
“Sio wajibu wenu kuwasuluhisha lakini ni wajibu wenu kuwashauri kwamba jamani ninyi ni wanandugu, halafu tena pengine ninyi ni majirani mgogoro wenu huu ninavyoona mnaweza kuumaliza tu kindugu au kifamilia maisha yakaendelea,’ amesema Mhe. Masaju.
Kadhalika, Jaji Mkuu amewaeleza Mahakimu hao kwamba Mahakama za Mwanzo kimsingi zilikusudiwa ziwe Mahakama za upatanishi na ndio maana makosa yote ya jinai yanayosikilizwa na Mahakama za Mwanzo yote yanadhaminika lakini pia hata mtu asiye na mdhamini anaweza akajidhamini.
“Na kwa sababu hiyo tumeelekeza kwamba Mahakama za Mwanzo zisipeleke watu Mahabusu na mpaka sasa hakuna hata Mahabusu mmoja wa Mahakama za Mwanzo katika Magereza yetu ya Tanzania, matumaini yetu ni kwamba nanyi mtaenda kuanzia hapo muendelee, msije mkasema mnakuja na ufundi fulani, makosa yote ya jinai yanayosikilizwa Mahakama za Mwanzo yanadhaminika, kama mtu ana wadhamini watamdhamini na kama amekosa wadhamini kwa namna yoyote ile aruhusiwe kujidhamini,” amesisitiza Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu amesema kwamba, kuna kanuni za msingi ambazo hawawezi kuzipuuza, hivyo ni muhimu Maafisa hao kuzingatia vitendea kazi vya utendaji kazi ikiwa ni pamoja kutenda haki na kujiridhisha kama haki imetendeka ‘sensitive to justice’, waweze pia kujiongeza, kuwa waadilifu, kujituma kufanya kazi, kuwa wabunifu ili kuimarisha ufanisi, kuwa na uzalendo wa Taifa.
Mhe. Masaju ameongeza kuwa, “Ibara ya 107B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nayo ni moja ya Kanuni zinazoongoza utendaji kazi wa Mahakama, nayo inasema, ‘Katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki, Mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia tu masharti ya Katiba na yale ya Sheria za Nchi.’
Ameeleza kwamba, uhuru huo unapatikana kwa kuzingatia mambo matatu ambayo ni pamoja na kuzingatia Katiba na Sheria za Nchi, kuzingatia maadili ya utumishi wa Maafisa wa Mahakama (Mahakimu na Majaji) na kuzingatia kiapo. Hivyo, amesema kwamba Maafisa hao wakishindwa kusimamia hayo watashindwa kuwa huru kutekeleza majukumu yao ya utoaji wa maamuzi.
“Kwa mfano kwa wale wanaokula rushwa, ukishakula rushwa una uhuru gani? Mtapendelea, ukisema huyu ni ndugu yangu ni kabila langu, sijui tunasali wote pamoja hapo tena huwezi kuwa huru, kwahiyo niwaombeni tunapata nguvu hii sisi ya kuwa kauli ya mwisho ya kutoa haki kwa sababu tunakuwa huru tunapokuwa tunafanya maamuzi,” amesisitiza Jaji Mkuu.
Amesema Serikali inachukua hatua za kuboresha maslahi ya Watumishi wa Mahakama, hivyo amewataka Mahakimu hao kwenda kufanya kazi kwa amani na kutoweka sababu mbalimbali ikiwemo mshahara mdogo kutokuwa kigezo cha kuchukua rushwa.
Aidha, Mhe. Masaju amewataka Mahakimu hao kutenga muda wao kusikiliza hotuba na maelekezo ya Viongozi wa Kitaifa wakiwemo Viongozi wa Kitaifa wa Mahakama ya Tanzania kwa sababu maelekezo yanapatikana kwenye Katiba, Sheria lakini pia yanapatikana kwa Viongozi wa Serikali ambayo inajumuisha Mahakama. Amewasisitiza pia Mahakimu kuisoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sambamba na kudumisha utawala wa sheria.
Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu amewasihi Mahakimu hao kuendelea kuwajali wazazi wao, wenza wao licha ya kuwa wamepata nafasi hiyo ambapo amesema, “Wakati mnaapa wengine nimewaona wana pete kuashiria kwamba ni wanandoa, sasa mafanikio haya mliyoyafikia leo yasije yakawatenganisha kwenye ndoa zenu, msifanye hivyo endeleeni kuheshimiana na wale ambao hamjapata ndoa endeleeni kujiheshimu mpaka hapo mtakapofikia hatua ya kuwa na ndoa lakini pia mtaendelea kujiheshimu maisha yenu yote.”
Baada ya hafla ya uapisho, Mahakimu hao wapya watapatiwa mafunzo elekezi ya siku 10 ili kupatiwa ‘abc’ za utendaji wa kazi ya uhakimu kabla ya kwenda kuanza kufanya kazi hiyo rasmi katika Vituo walivyopangiwa.
Chanzo: mahakama ya Tanzania