Madaktari Bingwa wa Samia Watajwa kuwa Chachu ya Huduma Bora za Afya

0


Na WAF- Tabora

Kampeni ya Madaktari Bingwa wa Rais Dkt. Samia nchini imetajwa kuwa chachu ya kupata huduma bora za afya kwa wananchi wa kipato cha chini bila kutumia gharama kubwa, kuokoa maisha na muda.

Hayo yamesemwa Septemba 29, 2025 na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Gerrard Mongela wakati akiwakaribisha Wataalam, Madaktari Bingwa na Bobezi wa Samia watakaotoa huduma za kibingwa katika Hospitali za Halmashauri nane za Mkoa wa Tabora kwa muda wa siku sita.

Mhe. Mongela ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuwezesha zoezi hilo kwa lengo la kuimarisha huduma za afya kwa wananchi wakiwa kwenye maeneo yao.

Amesema hali hiyo inasaidia kukuza uchumi wa eneo hilo na wananchi wake kwani fedha ambazo wangetumia kufuata matibabu mbali zinatumika katika matumizi mingine na kukuza uchumi binafsi.

“Napenda kuishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta wazo hili la kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi wa kipato cha chini wakiwa katika maeneo yao, hali hii inadhihirisha dhamira njema ya Mhe. Rais kuwajali wananchi wake,” amesema Mhe. Mongela.

Mhe. Mongela ameongeza kuwa, wananchi wa kipato cha chini huwa wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali ambayo yanahitaji huduma za kibingwa lakini kutokana na kutokuwa na uwezo ikiwa ni pamoja na kufuata huduma hizo mbali, wengi wao huishia kubaki wakiumwa hata kusabisha vifo.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Watoto Wachanga, Watoto na Vijana kutoka Wizara ya Afya Dkt. Felix Bundala amesema zoezi la Madaktari Bingwa wa Samia lina gharama kubwa lakini Serikali imeona ni bora liendelee kutokana na mrejesho chanya kutoka kwa wananchi kupata huduma za kibingwa katika maeneo yao.

Mganga Mkuu wa Tabora Dkt. Honoratha Rutatinisibwa amesema mkoa huo una madaktari bingwa 29 sawa na asilimia 21 za uhitaji hali inayopelekea ukosefu wa huduma za kibingwa lakini uwepo wa kambi za Madaktari Bingwa wa Samia umesaidia kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi ambapo kambi tatu zilizopita zilihudumia wananchi zaidi 5000 huku ikibainika magonjwa yasiyo ya kuambukiza kuwa kinara.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top