Na Ghati Msamba-Musoma
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Musoma Mjini kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Christina Ndengo, ameahidi kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo kwa uadilifu na uwazi, endapo watampa ridhaa ya kuwa Mbunge katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Chagangara, kata ya Kwangwa, Ndengo aliwaeleza wananchi mambo manne makubwa atakayoyatekeleza mara baada ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Musoma Mjini.
Alisema kipaumbele chake cha kwanza kitakuwa ni kuhakikisha ujenzi wa zahanati katika eneo hilo unakamilika, ili kupunguza gharama za huduma za afya kwa wananchi wenye kipato cha chini wasioweza kumudu matibabu katika hospitali za rufaa.
Ndengo alisisitiza kuwa afya ni haki ya msingi kwa kila mwananchi, hivyo atashirikiana na serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha huduma za afya zinapatikana karibu na wananchi wote, hususan katika maeneo ya pembezoni mwa mji.
Pia, aliahidi kufuatilia kwa karibu upatikanaji wa fedha za miradi ya barabara na kuhakikisha barabara zote za ndani ya mji wa Musoma zinajengwa kwa kiwango cha lami ili kuendana na hadhi ya manispaa hiyo.
Aidha, Ndengo alisema atashauri serikali kufufua na kuanzisha viwanda vipya vitakavyotoa ajira kwa vijana na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Musoma na taifa kwa ujumla.
Aliongeza kuwa sekta ya viwanda ikiboreshwa itasaidia kupunguza tatizo la ajira, kuongeza mapato ya serikali na kukuza uchumi wa wananchi kupitia uzalishaji wa bidhaa za ndani.
Katika sekta ya elimu, mgombea huyo alisema atahakikisha changamoto za wanafunzi wanaokomea darasa la sita zinapatiwa ufumbuzi kwa kushirikiana na wazazi, walimu na serikali ili watoto wote waweze kuendelea na masomo bila kukatishwa.
Alitoa wito kwa wananchi wa Jimbo la Musoma Mjini kumpa kura Oktoba 29 ili awawakilishe ipasavyo na kuhakikisha maendeleo yanayogusa maisha yao yanapatikana kwa vitendo, si maneno.
Aidha, Christina Ndengo aliwasisitiza wananchi wa Musoma Mjini kuendelea kuitunza ardhi na kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Alisema ardhi ikitunzwa vizuri itasaidia kuimarisha kilimo kinachozunguka Ziwa Victoria na kuwezesha uzalishaji endelevu wa mazao ya chakula na biashara.
Vilevile, alihimiza wananchi kujikita katika ufugaji wenye tija kama ajira mbadala kwa wakazi wa Musoma, akisisitiza kuwa bila kuongeza idadi ya mifugo bora, jamii inaweza kuingia kwenye hatari ya kukosa nyama, maziwa na mayai, ambavyo ni vyakula muhimu kwa afya ya binadamu. Aliongeza kuwa sekta ya kilimo na ufugaji ikiendelezwa ipasavyo, itasaidia kuinua kipato cha wananchi na kuchochea maendeleo ya uchumi wa jimbo hili.