Ujumbe wa Tanzania Washiriki Ufunguzi wa Mkutano wa 22 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje Afrika na Nordic

0


Ujumbe wa Tanzania unaoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, umeshiriki katika ufunguzi wa Mkutano wa 22 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje kati ya Afrika na Nchi za Nordic unaoendelea mjini Victoria Falls, Zimbabwe.

Mkutano huo umefunguliwa rasmi na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Zimbabwe, Prof. Amon Murwira, ambaye alisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi za Afrika na Nordic. Aidha, alibainisha kuwa mkutano wa mwaka huu unalenga kuchochea matumizi ya ubunifu na teknolojia katika maandalizi ya jamii endelevu.

Shughuli za siku ya kwanza ya mkutano huo zimejumuisha majukwaa mbalimbali ya mijadala. Miongoni mwao ni Jukwaa la Kibiashara la Afrika na Nordic lililojadili namna ya kufanikisha ustawi endelevu kupitia ushirikiano na kupunguza hatari za biashara. 

Aidha, Jukwaa la Vijana Wabunifu limeibua hoja kuhusu nafasi ya vijana kama chachu ya maendeleo endelevu kupitia teknolojia na mshikamano wa kijamii. Vilevile, Jukwaa la Wasomi limejadili mada ya “Kutoka kwenye Misaada kuelekea Biashara” likihimiza umuhimu wa kubadili mifumo ya ushirikiano kuelekea ushirikiano wa kibiashara unaonufaisha pande zote.

Katika Jukwaa la “Kutoka Misaada Hadi Biashara”, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi  Kombo, alisisitiza haja ya kuhakikisha thamani ya rasilimali za Afrika inakidhi maslahi ya Afrika na kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wake.

Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo unaendeleza utekelezaji wa diplomasia ya uchumi inayolenga kuimarisha biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kimataifa kwa manufaa ya Watanzania.






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top