Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari ameongoza kikao cha Timu ya Sheria ya Serikali (The Government Legal Team) kwa ajili ya kufanya uchambuzi wa kimkakati wa masuala ya kisheria, kuhusu huduma za kisheria zinazotolewa, uendeshaji wa mashtaka, pamoja na utoaji wa maamuzi ya kisheria.
Timu ya Sheria ya Serikali imekutana na kufanya kikao chake cha tisa kilichofanyika leo, Septemba 19, 2025, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa kikao hicho ni maalumu kwa ajili ya kujadili uchambuzi wa Kisheria wa kimkakati, huduma za kisheria zinazotolewa pamoja na huduma za uendeshaji wa mashtaka na utoaji wa maamuzi ya kisheria kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa.
Aidha, Mhe. Johari ameeleza kuwa ni muhimu kuendelea kuhuisha majukumu ya kisheria ili yaendane na utekelezaji wa misingi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayojumuisha Umoja, Utu, Haki za Binadamu, Demokrasia, Ulinzi wa Maliasili na Rasilimali, pamoja na Ulinzi wa Utamaduni na Maadili ya Taifa.
“Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili iweze kutekelezwa ipasavyo, ni lazima sheria zitungwe na kurekebishwa ili ziendane na malengo ya Taifa ya kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kati wa ngazi ya juu,” amesema Mhe. Johari.
Katika hatua nyingine Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa wito kwa washiriki wa kikao hicho kutoa maoni na mapendekezo yatakayowezesha sekta ya sheria nchini kuwa na mchango chanya katika maendeleo ya Taifa na kufanikisha malengo ya Dira ya Maendeleo 2050.
Kikao cha Timu ya Sheria ya Serikali kinahusisha Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi mbalimbali zinazotoa huduma za Kisheria nchini ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar, Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Tume ya Kurekebisha Sheria, Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini,(RITA) Mahakama pamoja na Chama cha Mawakili wa Serikali (TPBA).
Chanzo: ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali