📌 Jaji Mkuu asema ipo haja ya kufanya marekebisho ya Kanuni za uchaguzi
📌 Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman ashiriki kutoa uzoefu kuhusu mashauri ya uchaguzi
📌 Jumla ya washiriki 381 wanufaika na mafunzo hayo
Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Mafunzo ya Namna Bora ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi yaliyokuwa yakitolewa kwa Majaji, Naibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na za Wilaya nchini yamehitimishwa leo, huku Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akishauri kwamba Kanuni za Uchaguzi zifanyiwe marekebisho ili kuwawezesha Majaji na Mahakimu kusikiliza ipasavyo mashauri hayo.
Akizungumza tarehe 18 Septemba, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo hayo yaliyohusisha washiriki wa kundi la mwisho la Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Masaju amesema majadiliano mbalimbali pamoja na changamoto zilizowasilishwa na washiriki wa Mafunzo yameonesha kuwa, kanuni hizo zina mapungufu na hivyo kuwa na haja ya kuzifanyia mabadiliko.
“Niwashukuru kwa kukubali kufanya mabadiliko ya kanuni hizi zinazotungwa na Jaji Mkuu, tumepata ushauri mzuri hapa na Jaji Mkuu Mstaafu ametushauri maeneo ya kuangalia , tuna pa kuanzia na wawezeshaji wetu ni mahiri na ninyi wenyewe ni mahiri mna ustadi mkubwa kwenye maeneo haya na hili tutalifanya kabla ya tarehe ya uchaguzi wenyewe na litakuwa zoezi shirikishi lakini maboresho ya mwisho yatakayotolewa lazima yapate kibali cha Mahakama maana sisi ndio wenye ile sheria na mwenye mamlaka ya kuitunga ile sheria ni Jaji Mkuu,” amesema Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu ameeleza kuwa, lengo la kufanyia marekebisho kanuni hizo ni kwa sababu ni sheria za uchaguzi zimekusudia kufikia lengo la wananchi la kupata Serikali ambayo itawajibika kwao kwa ajili ya ustawi wao wananchi kama inavyotajwa kwenye Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo pamoja na mambo mengine inasema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na inayofuata haki ya kijamii na kwamba mamlaka ya Serikali hiyo yatapatikana kutoka kwa wananchi.
‘Na kwamba wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii na lengo kuu la Serikali ikiwa ni ustawi wa wananchi na Serikali ikiwajibika kwa wananchi,’ amenukuu Mhe. Masaju akirejea Ibara ya 8 ya Katiba.
Ameongeza kuwa, lengo lingine la kufanya maboresho kwenye kanuni hizo ni kuleta uwazi zaidi katika kupata tafsiri sahihi ya migogoro ya uchaguzi inayoletwa mahakamani na kujua kama uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.
Amesema kuwa, katika mazingira kama hayo, Mahakama ambayo ina jukumu la kutunga kanuni za kusimamia mashauri ya uchaguzi lazima ijiridhishe kama kanuni hizo zinakidhi matarajio ya wananchi ili watu wanaokuwa na mashauri ya uchaguzi mahakamani yaamuliwe kwa namna ambayo wanaridhika kwamba maamuzi hayo yamefanyika kwa kuzingatia Katiba na Sheria za nchi.
Ameeleza kuwa, baadhi ya changamoto zilizoonekana katika Kanuni hizo ni pamoja na kukosekana kwa uwazi na uhakika pamoja na mapungufu mengine yatakayobainika baada ya kuzipitia kanuni hizo.
Kufuatia maelekezo ya Jaji Mkuu kuhusu mabadiliko ya kanuni za uchaguzi, Majaji wa Mahakama ya Rufani kwa pamoja wamepanga kukutana Jumatatu tarehe 22 Septemba, 2025 ili kupitia kanuni hizo za uchaguzi na kutoa mapendekezo ya maboresho yake.
Aidha, Mhe. Masaju ameeleza kwamba, mashauri yanayotokana na migogoro ya uchaguzi yatasikilizwa katika Mahakama zilizopo nchini na kuwataka watu wanaohitaji kufuatilia mashauri hayo kufika katika Mahakama husika wasikilize kwa amani na kwa kufuata na kuheshimu taratibu za Mahakama. Ametoa rai kwa mtu ambaye hataridhika na uamuzi wa Mahakama ya ngazi fulani ana haki ya kukata rufaa kwa kuwa ni haki ya kikatiba.
Mhe. Masaju amesisitiza kuwa, Mahakama inalo jukumu la kudumisha utawala wa sheria katika nchi kwa mujibu wa Ibara ya 26 ya Katiba ambapo amethibitisha kwamba Mahakama itahakikisha inaendelea kufanya hivyo.
“Pamoja na mamlaka tuliyo nayo ya kikatiba na kisheria, mamlaka yetu pia yapo katika uwezo wetu wa kufanya maamuzi ya Mahakama kwa maslahi ya sheria, amesema Jaji.
Kadhalika, Jaji Mkuu ameeleza kwamba hakutakuwa na urushaji mubashara (live streaming) ya mashauri hayo na kusisitiza kuwa, “hakutakuwa na ‘live streaming’ ya mashauri hayo huku akirejea kinachozungumziwa kwenye Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa; ni haki ya kupata taarifa sio haki ya kutangazwa wakati wote.
Katika hatua nyingine amewashukuru waandaaji wa mafunzo hayo Mahakama na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, wawezeshaji pamoja na washiriki wote wa mafunzo hayo kushiriki kikamilifu.
“Nawashukuru washiriki wote, waandaaji na Wawezeshaji wa Mafunzo haya ambayo niliyafungua tarehe 28 Agosti, 2025 lakini katika ngazi mbalimbali, tulianza na Mahakama Kuu kwa pamoja, Naibu Wasajili, Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na za Wilaya, zoezi ambalo limefanyika kwa ustadi mkubwa sana,” amesema Mhe. Masaju.
Kwa upande wake Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman ametoa uzoefu wake kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani juu ya mashauri yatokanayo na migogoro ya uchaguzi ambapo ameshauri juu ya menejimenti fasaha ya mashauri ya uchaguzi kwa kuwa yanagusa Taifa, kuwa na matumizi fasaha ya lugha na mengine.
“Tuwajibike ipasavyo na tutumie uchaguzi huu kujiimarisha kama Mahakama kupitia maamuzi yetu kujenga ‘integrity’ ya Mahakama,” amesema Mhe. Chande.
Jaji Mkuu huyo Mstaafu amesisitiza mambo ya kuzingatia kuwa ni pamoja na Mahakama kuangalia Sheria na wajibu wake kwenye masuala ya uchaguzi, usikilizwaji wa mashauri ya uchaguzi mapema ipasavyo na Mahakama iwe na uwazi na yenye kufikika kwa kuwa mashauri hayo yana maslahi ya umma.
Mhe. Chande amesema, mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kwa kuwa uchaguzi na migogoro ya uchaguzi kwa kiasi kikubwa ni muingiliano kati ya siasa na sheria.
Majaji wengine walioshiriki kutoa uzoefu wao kuhusu mashauri ya migogoro ya uchaguzi ni Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Ferdinand Wambali na Mhe. Issa Maige.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto yalifunguliwa na Jaji Mkuu tarehe 28 Agosti, 2025 lengo likiwa ni kuimarisha uwezo wa Maofisa Mahakama, yaani Majaji na Mahakimu katika namna bora ya kuendesha mashauri ya uchaguzi ili kuwaweka tayari kushughulikia mashauri hayo kwa weledi na mapema ipasavyo pale ambapo wadaawa watakuwa wamegonga milango ya Mahakama kutafuta haki.
Kwa mujibu wa Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo mafunzo hayo yametolewa kwa jumla ya washiriki 381 wakiwemo Majaji wa Mahakama Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu, Naibu Wasajili, Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na za Wilaya.
Chanzo: mahakama ya tanzania