Na Angela Sebastian
Karagwe: Wilaya ya Karagwe kupitia wakala wa Barabara za vijijini na mjini TARURA imejipanga kuongeza mtandao wa Barabara za lami kutoka kilometa 25.29 hadi kilometa 28.29 ifikapo Novemba mwaka baada ya kikamilisha kilometa tatu za Lami katika mradi wa Barabara ya Nyakahanga -Nyabionza.
Mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2025 zimeweka jiwe la Msingi katika barabara hiyo ambayo Mradi wake umefikia asilimia 83
Meneja wa TARURA Wilaya ya Karagwe Kalembula Malimi amesema kuwa Serikali iliidhinisha shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya matengenezo ya Barabara hiyo kwa kiwango cha Lami na mpaka sasa mkandarasi amelipwa shilingi Bilioni 1.1
Amesema Barabara hiyo ni moja ya Barabara zinazochochea Uchumi wa wananchi na kurahisisha huduma za jamii.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa Ismail Ussi amewataka wananchi Kutumia Fursa za uwepo wa Barabara hiyo kufanya biashara kwa nyakati zote ili kukuza Uchumi wao na kuchangia Pato la Taifa.
Amesema Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Barabara za vijijini kwani ndiko kwa wananchi wanaotegemea kusafirisha mazao kwa ajili ya kujipatia kipato na kuendesha familia zao kupitia barabara bora na imara .
Kwa upande wa Meneja wa TARURA Wilaya ya Karagwe amesema kwa asilimia 78 Barabara zake zinapitia muda wote huku asilimia 22 Barabara zikiwa katika matengenezo na ukarabati wa mara kwa mara.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa,amemshuru Rais Dk .Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipatia Wilaya ya Karagwe fedha nyingi za maendeleo.
Bashingwa amesema kuwa Wilaya ya Karagwe imepiga hatua kubwa katika sekta ya afya kwa kuwa na Hospitali ya Wilaya yenye uwezo wa kutoa huduma zote muhimu, pamoja na vituo vya afya vilivyosambazwa katika tarafa zote za Wilaya hiyo,miradi ya barabara miundombinu ya elimu iliyoboreshwa na maji.