Na Ghati Msamba
Mara : Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amempokea Waziri wa Maji wa Kenya, Mhandisi Eric Mugaa pamoja na viongozi wengine kutoka nchini humo walioshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Mara (MARA DAY) yanayofanyika kila mwaka Septemba 15.
Kupokelewa kwa viongozi hao kumefanyika leo ofisini kwa Mkuu wa Mkoa mjini Musoma, ambapo walifanya mazungumzo kuhusu kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuboresha maandalizi ya kilele cha maadhimisho hayo yanayofanyika Wilaya ya Butiama, mkoani Mara.
Katika mazungumzo hayo, viongozi kutoka Kenya walipongeza Mkoa wa Mara kwa maandalizi mazuri, hususan miundombinu, mandhari ya kuvutia na upatikanaji wa chakula bora kwa wageni na washiriki wa maadhimisho hayo.
Kwa upande wake, Kanali Mtambi aliwahakikishia viongozi hao kuwa Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki itaendelea kudumisha mshikamano katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za Bonde la Mto Mara kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Baada ya kumalizika kwa mazungumzo hayo, msafara wa viongozi hao kutoka Kenya ukiongozwa na Mhandisi Mugaa ulielekea Wilaya ya Butiama kushiriki kilele cha sherehe za Siku ya Mara. Katika sherehe hizo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Mtambi, aliteuliwa kuwa mgeni rasmi.
Maadhimisho ya Siku ya Mara huwaleta pamoja wadau kutoka nchi za Tanzania na Kenya kwa lengo la kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kuhifadhi Bonde la Mto Mara, ambalo ni tegemeo kubwa kwa maisha ya binadamu, wanyamapori na shughuli za kiuchumi.