Na Angela Sebastian
Biharamulo : Mkuu wa mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwassa amesema kutokana na kampeni ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ya Kuhimiza matumizi ya Nishati safi na utunzaji wa mazingira, mkoa huo umeonyesha kwa vitendo utekelezaji huo ambapo wamegawa mitungi 1,054 ya gesi katika jamii.
Mitungi hiyo imegawiwa na kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Kitaifa 2025 Ismail Ali Ussi katika maeneo ambayo yana mkusanyiko wa kuanzia watu 100 na kuendelea ambayo ni ya binafsi na Serikali hususani shule,watu wenye mahitaji maalum na mama lishe.
Kwa upande wa kiongozi wa mbio za mwenge Kitaifa Ismail Ali Ussi ameendelea kuhamasisha uongozi wa mkoa huo na Wilaya zote kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi ya gesi na mbadala ili waepukane na matumizi ya nishati chafu ya kuni na mkaa ambayo huwasabishia madhara kiafya.
Aidha aliutaka uongozi wa mkoa huo hadi ngazi za chini kuendelea kuwaelimisha na kuhakikisha wananchi wa mkoa huo zaidi ya milioni1.7 waliojiandikisha katika daftari la mpiga kura wanajitokeza kupiga kura na kuchagu viongozi watakaowalatea maendeleo.
Mwenge huo ulianza mbio zake mkoani Kagera mnamo Septemba 7 na kuhitimisha leo Septemba 15 na kuelekea mkoani Kigoma ambapo umekimbizwa kilometa 1,040 , kuzindua,kufungua,kuweka mawe ya msingi,kikagua,na kutembelea miradi ya maendeleo 58 yenye thamani ya shilingi bilioni 23.8 ambapo yote imekubaliwa na mwenge .