Mkurugenzi wa Uratibu na Huduma za Ushauri wa Kisheria Bi. Neema Ringo kwa niaba ya Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa rai kwa Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutumia maarifa waliyopata kwa vitendo na kuhakikisha kuwa kila Ushauri wa Kisheria unaotolewa unalinda maslahi ya Umma na Taifa.
Hayo ameyasema leo tarehe 26 Septemba, 2025 katika kilele cha Mafunzo ya Mawakili wa Serikali wa Ofisi Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoka TANESCO.
Bi Neema Ringo aliwapongeza washiriki wote waliohudhuria mafunzo hayo kwani kupitia mafunzo hayo Mawakili wa Serikali watakuwa wameongeza maarifa katika kutatua changamoto.
“Hivyo, ni ukweli usiopingika kwamba kupitia mafunzo haya, Mawakili wetu watakuwa wamepata maarifa mapya na mbinu bora za kushughulikia changamoto zinazoweza kujitokeza, ikiwemo migogoro ya Kisheria, masuala ya udhibiti wa huduma na utekelezaji wa Mikataba mikubwa ya kimkakati kwa maslahi ya taifa.” Amesema Bi. Neema
Awali, akimkaribisha Mgeni Rasmi Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bi Lucy J. Benju, Meneja Uongozi na Uratibu aliushukuru Uongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuratibu mafunzo haya kwa Mawakili wa Serikali kwani kupitia mafunzo haya watadumisha ushirikiano na kuweza kuleta maendeleo ya jamii.
“Binafsi napenda kushukuru Uongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuratibu mafunzo haya yenye tija kwetu sote kwani lengo letu sote ni kuleta maendeleo kwa Taifa letu” amesema Bi. Lucy
Bi. Neema Ringo ameushukuru uongozi wa TANESCO na kushauri kuendeleza mafunzo haya mara kwa mara ili kujenga uwezo kwa Mawakili wa Serikali.
“Vilevile, Ninashauri kwamba TANESCO iendelee kuwekeza katika mafunzo kama haya ili kuendelea kujenga uwezo wa wataalamu wetu kwa kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.” Anasema Bi Neema Ringo.
Mafunzo haya yaliyotolewa kwa Mawakili wa Serikali yalianza tarehe 23 Septemba 2025 na kuhitimishwa leo 26 Septemba, 2025 katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere Kibaha, Pwani.
Chanzo: ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali