Na Emmanuel Chibasa
Kila binti wa
Kikurya anayekanyaga darasa la kwanza hubeba ndani yake ndoto kubwa ndoto ya maisha
yake ya baadae, lakini nyuma ya tabasamu na matarajio hayo, wingu zito la mila
ya ukeketaji hujificha, likisubiri kuzima ndoto hizo kwa kisingizio cha heshima
na maandalizi ya ndoa za utotoni.
Mara nyingine binti analazimishwa kuchagua kati ya elimu na ndoa, ama kati ya maisha ya ndoto yake na mateso ya kimila. Nikukaribishe katika simulizi ya matumaini na majonzi, inayoonesha namna haki na ndoto za wasichana zinavyopigwa vita katika jamii ya Kikurya kabila kubwa linalopatikana nchini Tanzania, Kenya na Uganda.
Ni majira ya saa kumi na mbili jioni nafika katika kijiji
cha nyamisisi kiabakari wilaya ya Butiama mkoani Mara Tanzania, na kutana na
Veronica Ryoba (sio jina lake halisi) msichana mwenye umri wa mika 18 sasa ambaye
ni miongoni mwa wasichana waliokimbia
familia zao kutokana na kulazimishwa kuolewa.
Veronika anasema alilazimika kukimbia familia yake na kwenda
kwa baba yake mdogo ambaye alimsomesha hadi darasa la 7 na baadae kutafuta
hifadhi katika kituo cha nyumba salama cha Hope for Girls and Women Tanzania
kilichopo wilaya ya Butiama mkoani Mara Tanzania.
Anasema mwaka 2020 akiwa na umri wa miaka 13 baba yake
mzazi alimlazimisha kukeketwa ili aweze kuolewa, na familia yao ipate mahari ambayo ingemsaidia mdogo wake wa kiume,
ambaye naye alikuwa anashawishiwa kuacha masomo ili aweze kutumia mahari hiyo
kuoa. Jambo ambalo mama yao alilipinga vikali.
Veronika anaeleza kuwa siku moja baba yao alirudi
nyumbani akiwa amelewa na alikuta mama yao hajamuachia chakula, hali
iliyosababisha ugomvi mkubwa hali iliyoplekea baba yao kuchukua panga na kumkamkata
na kumsababishia kifo mama yao.
Kutokana na huzuni ya kupoteza mtetezi baada ya kumalizika
kwa mazishi ya mama yao, Veronika aliamua kutoroka kwani baba yao aliendelea
kumlazimisha kukeketwa ili aolewe.
“Mwaka 2020 nilikimbia ukeketaji kwa sababu baba yangu
alikuaga mlevi sana na alikua anataka mimi nikeketwe ili niolewe apate mahari imsaidie mdogo wangu wa kiume kuoa na
kuendelea na maisha yake.
Nilipotoroka nilifika hapa nyumba salama nikapokelewa
vizuri na nikawaeleza changamoto
nilizopitia kule kijijini, wakanisaidia na nikafanikiwa kuanzia kidato cha kwanza hadi nikafanikiwa kuhitimu
mwaka 2024 kidato cha nne shule ya sekondari Kyabakari, nimefaulu vizuri na nategemea kuendelea na masomo yangu.”
Anasema Veronica
Ameongeza kuwa ukatili aliofanyiwa umeathiri pakubwa
maisha yake kwanza kama mzazi wake angefanikiwa kumkeketa asiwengeza kufikia
malengo yake ya kumaliza elimu ya msingi na sekondari.
Mbali na Veronica, Lucia Wambura ambaye pia sio jina lake
halisi, naye amekumbana na changamoto ya kulazimishwa kukeketwa na ndugu wa baba
yake ili aweze kuolewa mara tu baada ya kumaliza elimu yake ya msingi.
Lucia anasema tangu akiwa mdogo, baba yake alikua
anampenda sana na katika familia yao wazazi wake alisikia wakipinga mila ya
ukeketaji huku akiwasihi watoto wake ikiwa ni pamoja na dada zake wasome kwa
bidii, waweze kufaulu vizuri katika masomo yao na sio kukeketwa ili waolewe.
Anasema mara baada ya baba yake mzazi kufariki mwaka 2020, alishangaa kuona ndugu upande wa baba yake wakibadilika na kuonesha dalili za kuanza
taratibu za kutaka akeketwe mara baada ya kumaliza mtihani wa darasa la saba.
“ Kwa bahati mbaya
baba yangu alifariki mwaka 2020 nikiwa darasa la tatu, na baada ya hapo
nilianza kufuatiliwa na ndugu upande wa baba walitaka nikakeketwe. Yaani nilikua
naandaliwa kukeketwa baada ya kumaliza mtihani wa darasa la saba nilipogundua hila
yao nilitoroka nyumbani na kukimbilia kwa rafiki yangu ambaye tumemaliza nae
darasa la saba, ambapo mama yake alinipeleka dawati ambao walinileta hapa
nyumba salama ”
Lucia anasema ni ngumu kwake kuishi mbali na familia yake
kwani hakuwahi kudhani kuna siku ataishi mbali na familia yake lakini kwa sasa imetokea
na anaishi nyumba salama na mabinti wenzake.
“Kuondoka nyumbani pia kuliathiri masomo yangu maana muda
mwingine nikiwa nasoma nawaza nyumbani nakumbuka
familia yangu na ndugu zangu wengine niliowaacha kule nyumbani”
Nashauri jamii inayoendeleza mila ya ukeketaji iachane nayo,
kwa sababu inatuathiri sisi mabinti kisaikolojia, na pia waachane imani potofu
kuwa binti asiyekeketwa hawezi kuolewa na mwanaume wa kikurya.” Amesema Lucia.
Kwa miaka kadhaa mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na
wadau wengine wa maendeleo, yamekua yakishirikiana na serikali katika mapambano
dhidi ya ukatili wa kijinsia hususani ukeketaji, ndoa za utotoni na athari zake
kiafya kwa kutoa elimu pamoja na kutoa
msaada kwa wasichana wanaokimbia familia zao kutokana na kulazimishwa
kukeketwa.
Ripoti ya utafiti ya afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya Malaria Tanzania ya mwaka 2022, Inaonesha kuwa Mkoa wa Mara ni miongoni mwa mikoa mitano hapa nchini, inayoongoza kwa mimba za utotoni ambapo mkoa wa Songwe ndio unaongoza kwa kuwa na asilimia 45%, ukifuatiwa na mkoa wa Ruvuma wenye asilimia 37% Katavi ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na asilimia 34%, Mkoa wa Mara ukishika nafasi ya nne ukiwa na asilimi 31% na mkoa wa Rukwa ukishika nafasi ya Tano ukiwa na asilimia 30%
Katika Ripoti ya utafiti ya mwaka 2024 pia inaonesha mkoa
wa Mara unashika nafasi ya tatu kwa matukio ya ukatili wa kijinsia kwa kuwa na
asilimia 28, huku mikoa ya Arusha na Manyara ikiwa vinara wa matukio ya ukatili
wa kijinsia kwa kuwa na asilimia 43%
Hali hii inadaiwa kuchangiwa mila na desturi kandamizi kama
jambo la heshima na utambulisho wa ulinzi na ujasiri kwa mwanamke lakini kwa
undani wake, ni mfumo unaonyima wasichana haki ya kufanya maamuzi kuhusu miili
yao na maisha yao ya baadaye.
Visa kama hivi vinawapata wasichana walio wengi ambao
wanakumbana na changamoto kama hizi, lakini wanakosa fursa ya kupaza sauti zao
ili jamii iweze kuona jinsi mila hii inavyowathiri maisha yao na kushindwa kutimiza ndoto zao.
Rhobi Samwelly ni mkurugenzi
wa wa shirika la Hope for Girls and Women Tanzania lilioanzishwa kwa lengo la kupinga
na kuondoa ukatili katika jamii ambao pia kupitia mradi wa nyumba salama
zilizopo wilaya ya Butiama na Serengeti mkoani Mara, kwa ajili ya kuhifadhi
wasichana wanaokimbia vitendo vya ukatili, anasema jamii inawaona kama wasaliti
wanapo wasaidia wanawake na mabinti wanaofanyiwa
vitendo vya ukatili.
“ Wakati mwingine tunapotekeleza majukumu yetu tunatukana
changamoto ya watu kutukatisha tamaa, lakini
sisi tuandeleza mapambano ili kuhakikisha hili kundi linapata haki na kutimiza
ndoto zao na pia kuhamasisha vijana wa kiume kusoma kwa bidii ili na wao
watengeneze maisha yao Tunabadilisha mitazamo kwa vijana wa kiume kuwa wasiishi
kwa kuwategemea dada au wadogo zao wa kike kama vitega uchumi cha wao kupata
mahali ”
Rhobi ameongeza kuwa Jamii bado inahitaji elimu sana
kuhusu madhara ya vitendo hivi vya ukatili maana mabadiliko katika mila na
desturi yanakuja taratibu, na kuwataka wanahabari kuendelea kuibua visa na simulizi
ambazo hazizungumzwi katika jamii zetu ili wengine wapate kujifunza.
Itaendelea Sehemu ya Pili..