Mkoa wa Mara Kuandaa Maadhimisho ya Siku ya Mara kwa Usimamizi wa Uhifadhi

0


Ghati Msamba

Mara: MKUU wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amesema msukumo mkubwa wa hifadhi ya Bonde la Mto Mara unatokana na ukweli kwamba eneo hilo linahusisha milima, mito na baadhi ya mapori ya asili.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kanali Mtambi amesema utekelezaji wa uamuzi wa Mkutano wa 10 wa Afrika Mashariki ndio ulioanzisha maadhimisho ya Siku ya Mara (Mara Day) ambayo hufanyika Septemba 15 kila mwaka.

Amesema maadhimisho hayo yanatoa fursa nyingi, zikiwemo kukuza utalii na kuhamasisha utunzaji wa mazingira, ambapo kwa Mkoa wa Mara hoteli nyingi hujaza wageni na kuongeza idadi ya watalii katika Hifadhi ya Serengeti, hivyo kuimarisha utalii wa ndani na nje ya nchi.

“Mto Mara ni hazina kubwa. Unaanzia Mlima Mau nchini Kenya na kuishia Ziwa Victoria upande wa Tanzania, ambapo asilimia 60 ya mto ipo Kenya na asilimia 40 ipo Tanzania,” alisema Kanali Mtambi.

Aidha, alibainisha kuwa mto huo unachangia kuhifadhi Hifadhi ya Taifa Serengeti, ambayo ni urithi wa dunia unaojulikana kwa maajabu ya uhamaji wa nyumbu kutoka Serengeti kwenda Maasai Mara nchini Kenya wakati wa kiangazi. Kutokana na umuhimu huo, amesisitiza kuwekwa msukumo mkubwa wa uhifadhi wa mto huo.

Katika maadhimisho hayo, Kanali Mtambi alisema shughuli mbalimbali zitafanyika, ikiwemo upandaji wa miti 8,000 kwa ajili ya kuhifadhi mazingira. Pia vijiji 136 vinavyopakana na Mto Mara vitapatiwa elimu ya uhifadhi wa bonde hilo, pamoja na uwekaji wa vigingi vya mipaka ili wananchi watambue maeneo ya hifadhi.

Shughuli nyingine zitakazofanyika ni pamoja na kongamano la utafiti, maonesho ya shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi, pamoja na michezo.

Akijibu hoja za waandishi wa habari, Mkuu huyo wa Mkoa alisema serikali ya mkoa imekuwa ikichukua hatua madhubuti kuhakikisha changamoto zinazohatarisha vyanzo vya Mto Mara zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho hayo ili wapate elimu ya kutunza rasilimali hiyo muhimu, ambayo ni nyenzo ya maendeleo kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Maadhimisho ya 14 ya Siku ya Mara mwaka huu yatafanyika kuanzia Septemba 12 hadi 15 katika Wilaya ya Butiama mkoani Mara, yakiwa na kaulimbiu isemayo: “Hifadhi Mto Mara kwa Maendeleo Endelevu".

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top