Na WMJJWM-Dar Es Salaam
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amesema Tanzania imepiga hatua kubwa na muhimu za Kisera katika Malezi na Elimu ya Awali kwa Watoto Wadogo ikiwemo uzinduzi wa Program Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ya mwaka 2021.
Wakili Mpanju ameyasema hayo tarehe 9 Septemba, 2025 mkoani Dar Es Salaam wakati akifungua Warsha ya Wadau ya Kuimarisha Mbinu Jumuishi katika Malezi na Elimu ya Awali kwa Watoto Wadogo (ECCE) nchini Tanzania.
Wakili Mpanju amesema ili kutengeneza Tanzania yenye uchumi shindani, yenye nguvu inayoweza kushindana kimataifa na kutumia fursa za kimataifa kwenye majukwaa mbalimbali ni lazima Jamii na Wadau kuungana na Serikali katika kutekeleza DIRA 2050 kwa kuwekeza kwenye sekta ya elimu hususani malezi na elimu ya awali ili hatimaye tuweze kuchangia kwenye maendeleo ya Jamii na Taifa kwa ujumla.
Amesema pia Serikali katika Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 imesisitiza juu ya Elimu bora, ikiwemo elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kuwa ni muhimu kwa kuandaa rasilimali watu wenye maarifa, fikra bunifu na ujuzi katika maisha.
“Serikali imehakikisha shule zote za msingi zilizopo hapa nchini 20,386 zinakuwa na madarasa ya awali ambapo mpaka sasa tunayo madarasa ya awali 20,316 kwenye hizo shule. Hii ni hatua kubwa katika kutekeleza malengo endelevu na Mipango ya kitaifa.” amesisitiza Wakili Mpanju
Chanzo: wizara ya maendeleo ya jamii