Sehemu ya Pili
Na Emmanuel
Chibasa
Katika makala ya
awali tulishuhudia simulizi za huzuni na matumaini ya wasichana wa Kikurya
waliokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni ili kulinda ndoto zao, Hata hivyo simulizi
hizo hazijaishia kwao pekee, kwani tatizo la mila kandamizi bado linaendelea
kuathiri jamii na wadau wa maendeleo.
Licha ya juhudi za
serikali na wadau mbalimbali bado kunahitajika elimu ya kina ili kubadirisha
fikra kwa jamii juu ya mila zinazonyima wasichana haki ya kusoma, kuamua
mustakabali wao na kuishi maisha yenye utu.
Wakati vitendo vya
ukatili vikitajwa kupungua katika baadhi ya maeneo nchini, wataalamu na wadau
wa maendeleo wanashauri kuwa, bado mabadiliko ya kimila yanahitaji muda mrefu kufikiwa,
Wakieleza kwamba, mila na desturi zimejengeka kwa vizazi vingi, na mara
nyingine huchukuliwa kama chanzo cha heshima au utambulisho wa kijamii.
Waziri wa maendeleo ya Jamii,
Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt Dorothy Gwajima mwaka 2025 alitangaza
kushuka kwa matukio ya ukatili dhidi ya watoto na vijana ikilinganishwa na
utafiti uliofanyika mwaka 2009.
Akitangaza Matokeo ya utafiti
wa kitaifa wa ukatili dhidi ya watoto na Vijana ya mwaka 2024 tarehe 9 June 10,
2025 Mhe. Gwajima alisema, Matokeo ya utafiti wa
Machi-Juni, 2024 yanaonesha ukatili umeshuka kwa kiwango kikubwa ukilinganisha
utafiti wa 2009 ambapo, kwa watoto wa kike: Ukatili wa kingono umepungua kutoka
33% hadi 11%; Ukatili wa kimwili umepungua kutoka 76% hadi 24%; na Ukatili wa
kihisia umepungua kutoka 25% hadi 22%.
Kwa watoto wa Kiume: Ukatili wa kingono umepungua kutoka 21% hadi 5%; Ukatili wa kimwili umepungua kutoka 74% hadi 21% na Ukatili wa kihisia umepungua kutoka 31% hadi 16%.
Licha ya matokeo
hayo kuonesha kushuka kwa viwango vya ukatili dhidi ya watoto na vijana, wadau
wa maendeleo wanasema bado changamoto kubwa katika utekelezaji wa sheria na
mabadiliko ya kijamii.
Nollasko Mgimba ni
Afisa Miradi kutoka Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma, anasema kupungua ni ishara
nzuri ya mafanikio lakini hakumaanishi tatizo limekwisha, kwani changamoto ya
utekelezaji wa sheria, mitazamo ya jamii na hofu ya viongozi kupoteza nafasi
zao za uongozi bado inakwamisha mapambano ya kutokomeza ukatili.
Mgimba anasema
changamoto kubwa wanayokutana nayo kama wadau wa maendeleo ni kutokukubalika
kirahisi katika jamii, kwani mara nyingi watendaji wa mashirika ya kupinga
ukatili huonekana kama wapinzani wa mila na desturi ambazo jamii huzichukulia
kuwa vyanzo vya heshima na hata kipato. Hali hii husababisha baadhi ya
wanajamii kushikilia mila hizo kwa nguvu na kutotoa ushirikiano katika jitihada
za kutokomeza vitendo vya ukatili.
“Tunayo changamoto kwenye usimamizi wa sheria na sera zilizopo,
kwa sababu jambo hili ni la kimila, unakuta katika maeneo haya kuna viongozi
wengi wanaochaguliwa au kuteuliwa wanaotoka katika mazingira haya, Katika
mapambano haya wanakosa nguvu kubwa ya kusimamia sheria na sera zilizopo
kutokana na wao kuwa sehemu ya mila na desturi hizo na wanahofia kupoteza
nafasi zao za uongozi kwa kuchaguliwa au kuteuliwa ” Amesema Mgimba.
SMAUJATA ni kampeni ya kitaifa ya kupinga ukatili wa
kijinsia na ukatili kwa watoto nchini Tanzania inanyofanya kazi chini ya Wizara
ya Maendeleo ya Jamii , Jinsia, Wanawake na Watoto na Mkundi maalum. Joyce
James ni Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Mara, anasema bado kunahitajika elimu ya kina katika jamii kuhusu
madhara ya mila ya ukeketaji na ndoa za utotoni ili kuondoa imani potofu zinazowalazimisha
wasichana kuingia katika ndoa au kukeketwa bila ridhaa yao.
“Bado jamii inapaswa kupewa elimu zaidi kufahamu madhara ya ukeketaji na ndoa za utotoni, mfano unakuta msichana analazimishwa kukeketwa au kuolewa bila ridhaa yake wasichana hawa ukumbana na madhara mengi, wananyanyasika, wanakutana na vitendo vya kikatili sasa msichana kama huyu hawezi kufurahia maisha ya ndoa na hapa ndio tunatengeneza kizazi cha ma single mother wengi katika jamii yetu” Amesema Joyce
Naye Neema Ndoboka kaimu mkurugenzi idara ya maendeleo ya
jamii akizungumza wakati akifungua kikao cha wadau wanaotekeleza eneo la mila
na desturi katika Mpango wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na
watoto (MTAKKUWA) Septemba 17,2025 mkoani Dodoma, amesema serikali inaendelea
na juhudi za kuchochea maendeleo katika jamii kupitia afua mbalimbali ikiwemo
utoaji wa elimu juu ya masuala ya mila na desturi zisizofaa kupitia mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja
na kushirikiana na wadau wa maendeleo.
Amesema serikali inatambua na kuthamini mchango wa wadau
wa maendeleo katika kuleta na kupambana zaidi katika kutoa elimu kwa jamii ili
kufikia malengo ya mabadiriko katika
jamii, lakini suala la mila na desturi linachukua muda hivyo wanapaswa kutokata
tamaa.
Baada ya kufanya mahojiano na wadau hao wa maendeleo
nilibaki na maswali ya kujiuliza je, dini inasemaje kuhusu ukeketaji na ndoa za utotoni na kama mila na ndoa
hizi za utotoni zinatambulika kidini?
Nimezungumza na Sheikh Omari Ali Hamisi kutoka Masid Musoma,
anasema katika jamii kuna muingiliano wa mila ikiwa ni pamoja na mila ya
ukeketaji ambayo madhara yake ni makubwa kuliko faida na kupelekea pia
wasichana chini ya umri wa miaka 18 kuingia katika ndoa za utotoni.
Amesema ndoa kwa mujibu wa dini ya kiislamu na kwa mujibu
wa sheria za dini , ndoa ni ibada na mtu anapoingia kwenye ndoa ameingia kwenye
taasisi ya ibada na inaongozwa kwa kanuni zake.
“Tunapozungumzia ndoa za utotoni, tunazungumzia ndoa
ambazo ziko chini ya ule umri ambao unatambulika kisheria ima kitamaduni, au
sheria ya nchi au kwa madhehebu na imani tofauti tofauti.
Ili kutokomeza tatizo hili kwanza inapaswa kutolewa elimu
baina ya mtu na mtu, familia, kitongoji, kijiji na maeneo mbalimbali katika
jamii kuelimishana madhara yanayopatikana kuhusiana ukeketaji madhara ya
kiafya, kisaikolojia na kiuchumi yanayopatikana kutokana na ukeketaji na
ukatili wa kijinsia kwa wasichana na watoto.