Kituo cha Umahili MUHAS ni Nguzo ya Kuinua Utaalamu wa Afya Nchini- Prof Nombo

0


Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amezindua Kamati Tendaji ya  Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu kilichopo Mloganzila, kinachomilikiwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), ambapo amesisitiza umuhimu wa kuvilinda na kuvitunza vifaa vya kisasa vilivyopo kituoni hapo ili viendelee kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya sekta ya afya.

Katika ziara hiyo, Prof. Nombo alijionea vifaa vya kisasa vinavyotumika katika ufundishaji na ujifunzaji kwa lengo la kuboresha ujuzi wa wataalamu wa afya nchini. “Vifaa hivi ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya sekta ya afya. Ni wajibu wa MUHAS kuhakikisha vinatunzwa kwa uangalifu ili viendelee kutoa mchango mkubwa katika mafunzo ya wataalamu wetu,” alisisitiza.

Kituo hicho ni miongoni mwa jitihada za Serikali na wadau wa maendeleo katika kuboresha elimu ya afya na kuongeza ufanisi wa huduma za matibabu kwa wananchi.

Akizungumza katika kikao cha kwanza cha Kamati ya Uendeshaji ya Awamu ya Pili ya Mradi wa Kituo hicho, Prof. Nombo alieleza kuwa utekelezaji wa awamu hiyo utakuwa chachu ya kukuza ujuzi wa wataalamu wa afya nchini. Alisisitiza kuwa mradi huo ni ushahidi wa wazi wa namna Serikali inavyowekeza katika kuimarisha elimu ya afya na kuhakikisha taifa linapata wataalamu mahiri wa kutoa huduma bora kwa wananchi.

“MUHAS ni taasisi inayotoa utaalamu wa kisayansi na kuandaa wataalamu wa afya kwa kiwango cha juu. Kituo hiki ni mahali pa kufundisha mabingwa na bobezi katika sayansi ya moyo na mishipa ya damu. Tunaona vifaa vinavyotumika ni vya kisasa, hivyo tunatarajia wananchi kunufaika kwa kiwango kikubwa kupitia huduma zitakazotolewa hapa,” alisema Prof. Nombo.

Mradi huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa kitaalamu wa MUHAS katika kutoa mafunzo ya vitendo na huduma za kibingwa, sambamba na kuimarisha miundombinu ya kisasa kwa ajili ya tafiti na mafunzo ya afya ya moyo na mishipa ya damu.

Chanzo: wizara ya elimu sayansi na teknolojia







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top