Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na TANAPA wameadhimisha Siku ya Faru Duniani ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Same mkoani Kilimanjaro Septemba 22,2025.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa NEMC Kanda ya Kaskazini, Afisa Mazingira Mwandamizi Bw. Francis Nyamhanga amezungumzia kuhusu umuhimu wa Faru kwenye mfumo wa Ikolojia.
"Kwenye mfumo wa Ikolojia Faru husaidia kufungua njia kwa kuvunja miti kwa ajili ya Wanyama wengine wadogo kuweza kupata malisho lakini pia hula mbegu za mimea mbalimbali hivyo kupitia kinyesi chao husaidia kusambaza mbegu katika mifumo Ikolojia na kinyesi hicho pia hurutubisha mifumo ikolojia bila kusahau wanachangia kukuza pato la Taifa kwani Faru ni kivutio cha utalii" amesema Bw. Francis.
Afisa Uhifadhi wa TANAPA, Bw. Jackson Lyimo ameeleza namna wanavyowafikia Jamii kwa kutoa elimu ya Uhifadhi wa Faru.
"Hifadhi Ina programu maalumu inayofahamika kama Rafiki wa Faru ambayo inafikia Jamii kwa kuipa elimu ya jinsi ya Faru hawa walivyotoweka, walivyorejeshwa na jinsi wanavyolindwa na kuzalishwa katika Hifadhi hii. Hadi sasa tumefikia shule 120 na kuwafikia walimu na wanafunzi takribani 3,600 toka Julai 2022" amesema Mhifadhi Lyimo.
Katika kuadhimisha Siku hii pia wanafunzi kutoka shule mbalimbali wamefika katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kujifunza namna Uhifadhi wa Faru unavyofanyika. Maadhimisho ya Siku ya Faru Duniani hufanyika mnamo Septemba 22 kila mwaka kwa lengo la kuelimisha Umma kuhusiana na Uhifadhi wa Faru na kuwalinda dhidi ya ujangili.
Chanzo: NEMC