Gavana Tutuba:Taasisi Ambayo Haitasajili TAMFI au TAMIU Kufutwa

0


Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amezitaka Taasisi za Huduma Ndogo za Fedha Daraja la pili kujiunga na taasisi mojawapo kati ya Mwamvuli wa Taasisi Zinazotoa Huduma Ndogo za Fedha (TAMFI) na Umoja wa Taasisi Zinazotoa Huduma Ndogo za Fedha( TAMIU) ifikapo Mwishoni wa mwezi Desemba 2025.

Gavana Tutuba amesema hayo alipozindua Utaratibu wa Utekelezaji wa Hati ya Makubaliano ya Usimamizi Binafsi wa Sekta ya Huduma Ndogo za Fedha, kati ya Benki Kuu, TAMFI na TAMIU.

“Taasisi zote za Huduma Ndogo za Fedha Daraja la pili zinalazimika kujiunga na chama kimojawapo kati ya TAMFI au TAMIU ndani ya kipindi cha miezi 6 na zoezi hili linatakiwa kuanza kutekelezwa kuanzia leo tarehe 1 Julai hadi mwishoni mwa Desemba 2025. 

Taasisi ambayo itakuwa haijajisajili kufikia Desemba tutainyang’anya leseni”. Amesema Gavana Tutuba.

Amesema kuwa lengo la kuwataka watoa huduma hao kujisajili katika vyama hivi ni kuboresha utoaji huduma na kutatua changamoto mbalimbali zinazosababisha madhila kwa walaji wa huduma hizo.

Aidha, Gavana amesema kuwa utaratibu huu wa usimamizi binafsi  utahakikisha TAMFI na TAMIU zinasimamia utendaji wa taasisi zinazotoa huduma ndogo za fedha kwa kuzingatia kanuni zilizopo kwa lengo la kutokomeza changamoto mbalimbali katika sekta hiyo ikiwemo Mikopo Umiza.

“TAMFI na TAMIU watakuwa  na wajibu wa kusimamia mwenendo wa wanachama wao kwa kuzingatia kanuni bora za kimaadili, kuhamasisha utoaji wa elimu ya fedha kwa wateja, kusimamia na kuratibu mifumo ya kushughulikia malalamiko, Kuweka taratibu za uwajibikaji na uwazi katika utoaji wa huduma, na Kuwezesha utekelezaji wa kanuni na miongozo ya kiserikali,” Amesema.

Ameongeza kuwa Benki Kuu itaendelea kusimamia sekta hiyo kupitia utekelezaji wa sera, utoaji wa leseni, ulinzi kwa watumiaji wa huduma za fedha, ufuatiliaji wa  mwenendo wa jumla wa sekta, na itahakikisha inashirikianiana  kwa karibu na vyama hivyo ili kuhakikisha kwamba misingi ya makubaliano hayo yanatekelezwa kikamilifu.

Kwa upande wake, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Usimamizi wa Sekta ya Fedha), Bi Sauda Msemo, amesema ongezeko la taasisi ndogo za fedha nchini hadi kufikia 2,600 linamchango mkubwa katika kuongeza ujumuishi wa huduma za fedha nchini na kuendelea kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha.

“Benki Kuu inatambua na kuthamini mchango huu, na ndio maana tumeamua kuanzisha utaratibu wa usimamizi binafsi, utaratibu ambao unalenga kuboresha uwajibikaji na uwazi katika sekta ya fedha, kwa lengo la kuendelea kumlinda mtumiaji wa huduma za fedha,” Amesema Bi. Msemo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bw. Sadati Musa.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya TAMFI, Bi. Devotha Minzi pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha TAMI,  Bw. Juma Mnanka,wameipongeza Benki Kuu kwa kuja na utaratibu huu na wameahidi wataendeleza ushirikiano ili kuhakikisha sekta hiyo inaimarika.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top