Na Ghati Msamba-Arusha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete, ameshiriki na kuhutubia Kongamano lililoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) lililofanyika jijini Arusha, likiwa na lengo la kujadili nafasi ya Ununuzi wa Umma katika ukuzaji wa kampuni za wazawa na makundi maalum kwa maendeleo ya uchumi jumuishi katika zama za mabadiliko ya teknolojia na kidigitali.
Katika hotuba yake, Waziri Ridhiwani alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutambua na kuthamini mabadiliko chanya yanayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo pamoja na mambo mengine, yamelenga kuinua ustawi wa watu wenye mahitaji maalum.
Aidha, Waziri Ridhiwani aliainisha mambo sita makuu ambayo yamefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwawezesha vijana na watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi, likiwemo agizo la kisheria la kutenga asilimia 30 ya zabuni za ununuzi wa umma kwa ajili ya makundi maalum.
Vilevile, alitoa wito kwa wadau mbalimbali wakiwemo Madiwani, Wakurugenzi wa Halmashauri, Manispaa na Majiji kutoa elimu kwa jamii kuhusu uwepo wa fedha maalum zinazotokana na manunuzi ya umma.
Alisema changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni uelewa mdogo wa wananchi kuhusu fursa hizo, jambo linalosababisha kutotumika ipasavyo kwa rasilimali hizo.
“Ni muhimu elimu hii ikawafikia watu wote, kwani hatua hiyo itasaidia kuongeza ushiriki wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika kutumia fursa kama zile asilimia 10 zinazotengwa na Halmashauri kupitia mapato ya ndani,” alisema Waziri Ridhiwani.
Akimshukuru PPRA kwa kuandaa kongamano hilo, Waziri aliipongeza taasisi hiyo kwa kutambua umuhimu wa kujadili masuala ya ununuzi wa umma kwa mtazamo wa maendeleo jumuishi, akisisitiza kuwa mafanikio ya malengo haya ni sawa na kuwawezesha Watanzania wote kiuchumi.
Kongamano hilo limekusanya wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi, likiwa jukwaa muhimu la majadiliano kuhusu namna bora ya kutumia ununuzi wa umma kama nyenzo ya maendeleo kwa makundi yaliyo pembezoni kiuchumi.