Wavuvi wa Jimbo la Musoma Vijijini wameanza kuvuna samaki na Kuanza kupata Mapato ya uhakika kutokana na uvuvi wa samaki kwa kutumia vizimba.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya Mbunge Jimbo la Musoma Vijijini inaeleza kuwa, Mvuvi mmoja wa Kijiji Cha Kigera, Kitongoji cha Kurukiri Kwa Sasa ana Uwezo wa kuvuna samaki takribani Tani 40 kutoka kwenye vizimba vyake 4 vyenye upenyo wa mita 10.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa Masoko ya samaki wanaovunwa kutoka kwenye vizimba yapo, ambayo ni ya walaji na viwanda vya minofu ya samaki. Bei inaendana na ukubwa na uzito wa samaki, na kwa sasa ni kati ya Shilingi 7,000 na 10,000 kwa kilo moja.
Wataalamu wa uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wakiwemo wa TAFIRI, walishirikiana na NEMC kubaini maeneo mazuri yanayokidhi vigezo vya kufanya uvuvi wa vizimba ndani ya Jimbo letu.
Mbali ya mikopo nafuu iliyotelewa na Serikali yetu kwenye uvuvi wa vizimba, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo anaendelea kuwashawishi wavuvi wa Jimboni mwetu kwenda Benki za CRDB na NMB kuchukua mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya uvuvi wa vizimba. Mbunge huyo ameishawasiliana na Benki hizo mbili kuhusu mikopo hiyo.
Wavuvi na wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini wanaendelea kutoa shukrani nyingi kwa Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha njia, kwa vitendo, ya uwekezaji mkubwa kwenye uvuvi wa vizimba nchini mwetu - ahsante sana!
Jimbo la Musoma Vijijini lenye jumla ya Kata 21, lina Kata 18 zilizoko pembezoni mwa Ziwa Victoria. na uvuvi ni kazi inayoajiri watu wengi Katika Jimbo Hilo.