Na Ghati Msamba-Musoma
Serikali ya Mkoa wa Mara imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kusimamia kwa ufanisi rasilimali za kiuchumi zilizopo mkoani humo, hususan sekta ya madini, ili ziweze kuwanufaisha wananchi kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, wakati wa uzinduzi wa kongamano la maonesho ya madini yanayofanyika kuanzia Juni 3 hadi Juni 6, 2025, katika uwanja wa Mukendo, Manispaa ya Musoma. Maonesho hayo yanalenga kuutangaza Mkoa wa Mara kitaifa na kimataifa kuwa ni miongoni mwa mikoa inayoongoza katika sekta ya madini.
Kanali Mtambi amesema Mkoa wa Mara unashika nafasi ya pili kwa uzalishaji wa madini nchini, ukitanguliwa na Mkoa wa Geita. Alieleza kuwa serikali ya mkoa itahakikisha madini yanachangia kikamilifu katika kuwaletea maendeleo wachimbaji na wananchi kwa ujumla.
"Katika maonesho haya, kutakuwa na kongamano litakalowapa wachimbaji elimu ya kina kuhusu madini, uchenjuaji, namna ya kuomba leseni, na matumizi ya teknolojia katika shughuli za madini. Vilevile kutakuwa na matembezi ya kuenzi kazi kubwa iliyofanywa na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake," alisema Kanali Mtambi.
Aidha, amewahimiza wachimbaji na wananchi wanaonufaika na sekta ya madini kuwekeza katika miradi ya maendeleo ndani ya Mkoa wa Mara, badala ya kupeleka mitaji yao katika mikoa mingine, ili kuupa mkoa huo heshima na ustawi wa kiuchumi.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Mara (MAREMA), John Marecho, amesema kuwa kongamano hilo litakuwa chachu ya mageuzi chanya kwa wachimbaji, likiwa jukwaa la kutatua changamoto na kuimarisha utendaji kazi wao.
Naye Mwenyekiti wa Wachimbaji Madini Wanawake Wilaya ya Butiama, Monica Mwita, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwapa leseni wanawake na hivyo kuwapa heshima kupitia uchumi wanaoupata kutokana namapato yatokanayo na madini.