Angela Sebastian-Bukoba
Mkazi wa kitongoji kijiji cha Mwanga wilaya ya Biharamlo mkoani Kagera Emmanuel Barakanfitye maarufu kama rais (52) amehukumiwa kunyongwa hadi kufa katika mahakama kuu kanda ya Bukoba baada ya kupatikana na kosa la mauaji ya mama yake mzazi aliyejulikana kwa jina la Mariana Matabaro.
Mawakili upande wa Jamhuri katika kesi hiyo walikuwa ni Matrida Assey pamoja na Gloria Lugeye.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwakwe mjini Bukoba,Wakili wa Serikali Matrida Assey amesema kuwa, hukumu hiyo imetolewa Mei 30,2025 baada ya mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa pande wa Jamhuri pasipo kuacha shaka lolote hivyo kumtia hatiani na kumuhukumu kifungo cha kunyongwa hadi kufa.
Amesema tukio hilo la mauaji ya Mariana Matabaro (75) lilitokea Mei 13, 2020 ambapo aliuawa na mtoto wake wa kumzaa Emmanuel akishirikiana na mshitakiwa wa pili Jackson Emmanuel (21) ambaye alikuwa mjukuu wa marehemu ambapo kijana huyo wakati wa tukio alikuwa na miaka (16).
Assey akizumgumzia tukio hilo alitaja sababu kubwa ya mauaji hayo kuwa ni ugomvi wa ardhi.
Ameongeza kuwa, mashuhuda ambao pia ni watoto wawili wa marehemu ambao ni Mambo Barakanfitiye na Goerge Barakanfitiye ambao wanaishi hatua 10 kutoka kwenye nyumba ya alipokuwa anaishi mama yao huyo marehemu siku ya tukio saa 2:00 usiku walikuwa wamekaa nje wanaota moto wakasikia kelele.
"Kelele zilikuwa ni za mama yao za kuomba msaada anaita nisaidie nisaidie wakati wanasikia kelele ghafla walimuona mama yao anatoka ndani anakimbia kuelekea kwenye nyumba za hao watoto wake" amesema Wakili Assey
Ameongeza kuwa, wakati watoto hao wanaota moto walikuwa na tochi hivyo waliposikia kelele wakaanza kumulika na kumuona kaka yao ambaye ni Emmanuel akiwa na mtoto wake Jackson na mtu mwingine ambaye hawakumtambua kwa sababu alikuwa amejificha wakiwa wanamfukuza marehemu.
"Wakati anawamulika walikuwa karibu ambapo kijana wa marehemu aitwaye Mambo alitaka kwenda kumsaidia mama yake kabla hajaenda akamuona Emmanuel akiwa ameshika panga na huku akimkata mama yake kichwani wakati huo Mambo akiwa na mdogo wake aitwaye Goerge"
"Wakati Mambo akielekea kumsaidia mama yake ndipo mshitakiwa wa pili Jackson akachukua jiwe na kumpiga nalo Mambo kifuani na mkononi akadondoka chini akawa ameshindwa kutoa msaada kwa marehemu, Goerge alipoona Mambo ameishapigwa na wenzake wana siraha akaogopa akakimbia anapiga kelele kuita watu waje kutoa msaada" amesema Assey
Amesema wakati Mambo akiwa amelala chini alikuwa anaona mama yake anaendelea kushambuliwa kwa mapanga na na kuendelea kutokwa damu nyingi ambapo wale wauaji waliondoka na baadaye walirudi na kuhakikisha amekata roho na Goerge ambaye alikimbia alipiga simu kwa mwenyekiti wa kitongoji cha Karundi A Petro Bukuku ili kuomba msaada.
Baada ya mwenyekiti kupata taarifa hizo alifika eneo la tukio na kupiga simu kituo cha polisi Biharamlo ambapo usiku huo wananchi waliendelea kulinda mwili na wengine walienda kuwatafuta wauaji.
Amesema walipofika kwa mke mdogo wa Emmanuel aliwambia alifika nyumbani akiwa na wasiwasi akaondoka na walivyoenda kwa mke mkubwa wa Emmanuel kumuulizia Jackson alisema hayupo nyumbani ameondoka.
Aidha wauaji hao baada ya kukamatwa na kufikishwa mahakamani mtuhumiwa wa kwanza Emmanuel alitiwa hatiani na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa huku Jackson ambaye wakati anatenda kosa alikuwa ni mtoto hivyo atakaa gerezani mpaka atakapotoka kwa msamaha wa Rais.
Hata hivyo kesi hiyo imehukumiwa na Jaji wa mahakama kuu kanda ya Bukoba Lilian Itemba.