Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki Kongamano la vijana kuhusu hifadhi na usimamizi wa mazingira, lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa maktaba mpya ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam Juni 3, 2025.
Mgeni rasmi katika Kongamano hilo alikuwa ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb).
Katika hotuba yake Mhe. Kassim Majaliwa amesema katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kitaifa mwaka huu, kutakuwa na midahalo itakayohusisha makundi mbalimbali kuhusu utunzaji wa mazingira kwa kudhibiti uchafuzi utokanao na taka za plastiki.
Amesema maadhimisho hayo kitaifa yanatarajiwa kufanyika Siku ya Mazingira Duniani ambayo ni June 5, 2025 mkoani Dodoma, yakiwa na kauli mbiu ya kitaifa inayosema 'Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo, Tuwajibike Sasa, Dhibiti Matumizi ya Plastiki'.
Waziri Mkuu Majaliwa ameongeza kuwa mdahalo huo kuhusu utunzaji wa mazingira utakusanya maoni yatakayoiwezesha Serikali kuongeza uwezo pamoja na kufanya marekebisho ya sheria na kanuni zitakazosimamia mazingira nchini.
Chanzo: Nemc Tanzania