Kamati ya Shule ya Msingi Mwisenge
“A”, iliyopo Manispaa ya Musoma mkoa wa Mara kwa kushirikiana na walimu pamoja na wazazi, imeweka mikakati mbalimbali
ya kuboresha kiwango cha ufaulu wa wanafunzi kwa mwaka 2027, ikiwa ni pamoja na
kukamilisha mitaala kwa wakati, kuanzisha masomo ya ziada na kuhakikisha wanafunzi
wanapata chakula wakati wa maandalizi ya mitihani.
Akizungumza katika kikao cha pamoja
na wazazi kilicholenga kujadili maendeleo ya taaluma shuleni hapo, Mwenyekiti
wa kamati Chrisant Nyakitita, amesema mikakati hiyo inalenga kuongeza
ufanisi wa ufundishaji na ujifunzaji pamoja na kuwahamasisha wazazi kushiriki
kikamilifu katika maendeleo ya elimu ya watoto wao.
Amesema shule imepanga kuanzisha
masomo ya ziada baada ya shule kufunguliwa kwa wanafunzi wa darasa la pili na
la nne hadi la saba, hatua inayolenga kuwasaidia wanafunzi kuimarisha uelewa
wao katika masomo mbalimbali.
Ameongeza kuwa mkakati mwingine ni
kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula wakati wa maandalizi ya mitihani ili
kuwawezesha kuwa na utulivu na kuzingatia masomo yao.
Gdfrey Masawa ni mwalimu wa taaluma
katika shule hiyo, awali akitoa tathmini
ya matokeo ya wanafunzi, amesema darasa la kwanza limeonesha ufaulu wa daraja
A, huku madarasa ya tatu na sita yakifikia kiwango cha daraja C, hali
inayohitaji juhudi zaidi katika kuboresha matokeo.
Akizungumzia matokeo ya mtihani wa
darasa la saba mwaka 2026, Masawa amesema jumla ya wanafunzi 84 walifanya
mtihani huo na shule kupata wastani wa alama 166.7, huku wanafunzi 79 sawa na
asilimia 94 wakipata madaraja A hadi C..
Ameeleza kuwa, katika matokeo ya
mtihani wa kitaifa wa darasa la saba mwaka 2025, shule hiyo ilipata wastani wa
alama 184 huku wanafunzi 16 wakishindwa kufikia kiwango cha ufaulu, wakiwemo
wavulana sita na wasichana 10.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa
shule hiyo Rosemary Lobozi, amesema katika kufanikisha mkakati wa ufaulu,shule
imepanga kuhakikisha mitaala inakamilishwa kwa wakati, kuimarisha masomo ya
ziada na kuboresha upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Amesema wazazi wana wajibu wa kufuatilia maendeleo ya taaluma
kwa watoto wao kushirikiana na walimu kuhakikisha changamoto za ujifunzaji
zinabainika na kutafutiwa ufumbuzi mapema badala ya kuwaachia walimu pekee huku
pia akitoa wito kwa wazazi kutowaacha watoto kuangalia televisheni muda mrefu
badala ya kujisomea..
Kwa pamoja, uongozi wa shule na
wazazi wamekubaliana kutekeleza mikakati hiyo kwa ushirikiano ili kuboresha
mazingira ya kujifunzia na kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi mwaka 2027.
Katika kuhakikisha mikakati huo
unatekelezeka kwa ufanisi, wazazi pamoja na uongozi wa shule wamekubaliana
kushirikiana kuhakikisha upatikanaji wa chakula shuleni. Kwa makubaliano hayo,
wazazi wamekubali kuendelea kuchangia
chakula kwa wakati ili kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma hiyo kwa wakati na
hivyo kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika masomo na maandalizi ya mitihani.
Imeandikwa
na Emmanuel Chibasa.


