Mgodi wa Barrick North Mara wazindua mashindano ya michezo kuimarisha mahusiano na vijiji 11

0


Na Ghati Msamba, Nyamongo – Tarime.

MGODI wa dhahabu wa Barrick North Mara umezindua mashindano ya michezo kwa lengo la kuimarisha mahusiano, mshikamano na ushirikiano kati ya mgodi huo na wananchi wa vijiji 11 vinavyouzunguka.

Uzinduzi huo umefanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Ingwe, Nyamongo, Wilaya ya Tarime, ambapo viongozi mbalimbali wameeleza kuwa michezo ni nyenzo muhimu katika kujenga umoja, kudumisha amani na kuimarisha mahusiano kati ya mgodi na jamii inayouzunguka.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, ameushukuru uongozi wa mgodi huo kwa kuanzisha mpango huo, akisema michezo ina nafasi kubwa katika kuwaunganisha wananchi na kujenga mahusiano mazuri.

Aidha, amewataka viongozi wa kimila kushirikiana na jamii katika kudumisha amani, umoja na mahusiano mema kati ya wananchi na mgodi.

Pia amewataka vijana kuacha tabia ya kuvamia maeneo ya migodi, akisisitiza kuwa shughuli za uchimbaji madini ni muhimu katika kuchangia mapato ya wananchi na Serikali, ambayo hutumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesema uzinduzi wa Wiki ya Mahusiano unalenga kuimarisha ushirikiano kati ya mgodi na jamii katika shughuli za kiuchumi, pamoja na kudumisha amani na usalama kwa kila mtu bila kujali tofauti za dini, rangi au kabila.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC), Rashid Bugomba, amesema michezo hiyo itaendelea katika vijiji husika baada ya uzinduzi ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuimarisha mahusiano yao na mgodi.

Ameeleza kuwa ni muhimu kwa wananchi na uongozi wa mgodi kushirikiana kutafuta suluhisho la changamoto ya uvamizi katika eneo la mgodi ili kuwezesha shughuli za uzalishaji kuendelea kwa usalama na kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii, CSR, unaendelea.

Naye Meneja Mkuu wa mgodi huo, Stephen Doyle, amesema michezo ina mchango mkubwa katika kukuza vipaji, kufungua fursa za ajira na kuwawezesha vijana kujipatia kipato.

Hata hivyo, ameeleza kuwa bado kuna changamoto ya uvamizi katika eneo la mgodi, huku akiwataka wazazi na jamii kwa ujumla kushirikiana kukabiliana na hali hiyo.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) unategemea shughuli za uzalishaji wa dhahabu, na kwamba mgodi utaendelea kushirikiana na jamii katika kutekeleza miradi yenye tija na manufaa kwa wananchi.

Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top