Wataalamu wa Afya Mazingira Wasisitizwa Kuzingatia Maadili ya Kazi

0


Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Eliud Eliakimu, amesisitiza umuhimu wa Wataalamu wa Afya ya Mazingira kuzingatia maadili ya kitaaluma katika utekelezaji wa majukumu yao, akieleza kuwa maadili ni msingi muhimu wa kuhakikisha taaluma hiyo inatekelezwa kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji.

Dkt. Eliakimu ameyasema hayo leo, Oktoba 26, 2026, jijini Dodoma, wakati wa mafunzo ya siku moja kwa Watarajali wa Afya ya Mazingira, ambapo amewataka kuzingatia misingi ya taaluma yao katika utendaji wa kazi na utoaji wa huduma kwa jamii.

"Mkiwa kama watarajali mnapaswa kuzingatia heshima, uadilifu na uwajibikaji wanapotekeleza majukumu yenu, tabia na mwenendo wenu wa kitaaluma vina mchango mkubwa katika kulinda hadhi ya taaluma na kuimarisha pimani ya wananchi kwa wataalamu wa afya," amesema Dkt. Eliakimu

Aidha, amewataka kutunza siri za taarifa wanazozipata katika utekelezaji wa majukumu yao ya kitaaluma na kuepuka vitendo vinavyoweza kushusha hadhi ya taaluma ya Afya ya Mazingira.

Ameeleza kuwa Wataalamu wa Afya ya Mazingira hufanya kazi katika mazingira mbalimbali na kukutana na wananchi wenye mahitaji tofauti, viongozi pamoja na wataalamu wa kada nyingine. Hivyo, ni muhimu kwao kuonesha weledi, kuheshimu wengine na kuzingatia maadili katika mazingira yote ya kazi.

Vilevile, Dkt. Eliakimu amesisitiza kuwa maadili ya kitaaluma yanapaswa kwenda sambamba na maarifa na ujuzi wanaoupata wataalamu hao kupitia mafunzo, ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kuzingatia misingi ya taaluma yao.

Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa kuzingatia maadili ya kitaaluma ni hatua muhimu katika kuboresha huduma zinazotolewa kwa jamii, kulinda maslahi ya wananchi na kudumisha heshima ya taaluma ya Afya ya Mazingira.

✍🏻wizara ya afya





Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top