Na Mwandishi wetu, Butiama
JUMUIYA ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Butiama imetakiwa kuendelea kudumisha umoja na mshikamano ili kuimarisha maendeleo ya jumuiya hiyo na chama kwa ujumla.
Wito huo umetolewa Oktoba 4, 2026 na Mjumbe wa Baraza Kuu la UWT Taifa Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly, aliyekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Butiama, Dkt. Charles Mahera, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya UWT Wilaya ya Butiama yaliyofanyika katika jengo la nyumba ya Katibu wa UWT lililopo, Kata ya Kukirango Wilayani Butiama.
Maadhimisho hayo, yameenda sambamba na kuchangia ujenzi wa jengo hilo ambalo kwa sasa lipo katika hatua ya upauaji.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Rhobi amesema umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama na viongozi wa jumuiya hiyo ni nguzo muhimu ya maendeleo na uhai wa jumuiya na Chama Cha Mapinduzi.
"Ushirikiano utaendelea kuifanya Jumuiya kupiga hatua mbalimbali, ikiwemo kukamilisha ujenzi wa nyumba ya katibu. Pia utaendelea kukifanya chama chetu kizidi kuwa imara katika kushika dola na kuwatumikia Watanzania kwa kuwaletea maendeleo," amesema Rhobi.
Aidha, amewataka wananchi kuwakemea wanaohubiri chuki, mafarakano na utengano miongoni mwa Watanzania, akisisitiza kuwa watu hao hawana nia njema na taifa.
"Tuwakemee wale wanaohubiri chuki, mafarakano na utengano miongoni mwa Watanzania kwani hawana nia njema. Toeni taarifa mapema mnapoona watu wanataka kuleta uvunjifu wa amani katika maeneo yenu ili amani iliyopo iendelee kudumishwa," amesema.
Pia ameitaka jumuiya hiyo kuyasema bila woga maendeleo yanayofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku akihimiza Watanzania kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Butiama, Christopher Marwa Siagi, amesema UWT ni Jumuiya muhimu ya chama katika kuimarisha uhai wa Chama cha Mapinduzi. Na amezitaka jumuiya zote za chama wilayani humo, kuhakikisha zinakamilisha ujenzi wa nyumba za watumishi ili kuwawezesha kupata makazi bora.
Katika kufanikisha ukamilishaji wa nyumba hiyo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Butiama, Christopher Marwa, amechangia Shilingi 500,000, huku Mbunge wa Butiama, Dkt. Charles Mahera, akichangia Shilingi 500,000 pamoja na mbao za kuezekea jengo hilo. Mjumbe wa UWT Taifa Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly, ameahidi kuchangia fedha ili kufanikisha upauaji huo.
Awali, Katibu wa UWT Wilaya ya Butiama, Ester Tuma, akisoma taarifa ya ujenzi, amesema ujenzi wa jengo hilo ulianza mwaka 2023 katika kata ya Kukirango ukiwezeshwa na viongozi wa Jumuiya hiyo Wilaya ya Butiama na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi.
Amesema, hadi sasa ujenzi huo umegharimu zaidi ya Shilingi milioni 15, likiwa katika hatua ya upauaji. Na ujenzi wote unatarajiwa kugharimu Shilingi milioni 52.4.








