Na Mwandishi Wetu, Musoma
MKUU wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Mtambi, amewapongeza Maafisa kutoka Ubalozi wa Poland nchini Tanzania na Wizara ya Mambo ya Nje ya Poland kwa msaada unaotolewa na serikali ya Pond kwa Shirika lisilo la kiserikali la Hope for Girls and Women in Tanzania la Mkoani Mara.
Shirika hilo, linajihusisha na kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia mkoani humo, ukiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni.
Pongezi hizo amezitoa Oktoba 28, 2026 ofisini kwake mjini Musoma, wakati akizungumza na maafisa hao waliopo mkoani Mara kukagua miradi inayofadhiliwa na Serikali ya Poland kwa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania na Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma kupitia Parokia ya Kiabakari.
Miradi inayofadhiliwa na Poland kwa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania inalenga kupambana na ukeketaji na ndoa za utotoni, ambapo shirika hilo limefanikiwa kujengewa nyumba salama kwa ajili ya kutoa hifadhi kwa wasichana wanaokimbia ukatili huo kutoka katika familia zao.
Pia, kusaidia kuimarisha utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya ukeketaji katika kuhakikisha watoto wa kike wanaendelea kutimiza ndoto zao. Mambo ambayo BrigediaJenerali Mtambi amesema, yanamchango katika kuwafanya watoto wa kike wawe na ustawi bora.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa aliwaomba maafisa hao kuwahimiza wawekezaji kutoka nchini Poland kuja kuwekeza ndani ya Mkoa wa Mara kwani mkoa huo unazo fursa nyingi, ikiwemo katika sekta ya madini, kilimo, uvuvi, utalii, fukwe na Makumbusho ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere Wilayani Butiama.
Akizungumza na Musoma News Hub, Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly, amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Mtambi, kwa juhudi na mikakati mbalimbali anayoifanya kuhakikisha anakomesha vitendo vya ukeketaji kwa watoto wa kike na kuweka mazingira bora ili watimize ndoto zao.
"Mkuu wa Mkoa amekuwa akihimiza ushiriki wa kila kiongozi kwa nafasi yake na jamii kwa ujumla, katika kupambana na ukeketaji na ndoa za utotoni kupitia vikao mbalimbali. Pia amekuwa karibu kutoa ushirikiano kwa mashirika yanayofanya miradi mbalimbali ya kupambana na ukatili na pia kusimamia maendeleo ya mkoa akihimiza uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi," amesema Rhobi.
Naye Naibu Balozi wa Poland Nchini Tanzania Daria Jankeil, akizungumza katika Kituo cha Nyumba Salama Kiabakari, alipongeza juhudi zinazofanywa na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania. Alisema, zinalengo la kuchochea maendeleo chanya ya watoto wa kike, na kuifanya kesho yao iwe na mafanikio.



.jpg)





