Wananchi Zaidi ya 5,000 Bumai Waondokana na Adha ya Kutafuta Maji

0


Na Angela Sebastian 

Zaidi ya wananchi 5,000 wa Kijiji cha Bumai, chenye vitongoji 14 katika Kata ya Kishanje, Wilaya ya Bukoba, wameondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata maji, baada ya kukamilika kwa mradi wa maji wa Bumai wenye thamani ya shilingi milioni 870.5.

Mradi huo umezinduliwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwango’nda, ambaye amewataka wananchi kutunza miundombinu ya maji na kulinda mradi huo ili uweze kudumu na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi kwa muda mrefu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Wazo amesema Serikali inaendelea na juhudi za kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji katika vijiji vyote nchini, ikiwa ni pamoja na kufikisha huduma hiyo kwa asilimia 85 na kuhakikisha wananchi wanaunganishiwa maji moja kwa moja majumbani ili kuwawezesha kutumia muda mwingi katika shughuli za kiuchumi na maendeleo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa na Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Evaristo Mugaya, mradi huo umekamilika na tayari wananchi wa Bumai wameanza kunufaika na upatikanaji wa maji safi na salama.

Mugaya alisema miongoni mwa miundombinu iliyojengwa katika mradi huo ni tanki kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi lita 100,000 za maji, vituo 11 vya kuchotea maji, uunganishaji wa maji katika kaya 100, mtandao wa mabomba wenye urefu wa kilomita kadhaa, mnara wa maji wenye urefu wa mita tisa, matenki ya kukusanyia maji pamoja na ofisi za Jumuiya ya Watumia Maji na Usafi wa Mazingira (CBWSO).

Alisema mradi huo umetokana na ukusanyaji wa maji ya chemchemi kutoka katika vitongoji vya Buhinda na Bugandika, hatua iliyowezesha kusambaza huduma hiyo kwa wananchi wengi zaidi na kupunguza utegemezi wa vyanzo vya maji visivyo salama.

Kukamilika kwa mradi huo kumepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya upatikanaji wa maji katika Kijiji cha Bumai na maeneo jirani, huku pia kukitarajiwa kupunguza magonjwa ya mlipuko yaliyokuwa yakijitokeza mara kwa mara kutokana na matumizi ya maji yasiyo salama.

 




Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top