Mwandishi wetu, Musoma.
MASHIRIKA yasiyo ya Kiserikali (NGOs) mkoani Mara yametakiwa kubuni vyanzo vya ndani vya mapato vitakavyoyawezesha kuwa na uendelevu katika utoaji wa huduma kwa jamii.
Hayo yamesemwa Septemba 29, 2026 na Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly, ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Taifa la NGOs Mkoa wa Mara, wakati akitoa salamu za Baraza hilo katika Jukwaa la Mwaka la mashirika hayo.
Jukwaa hilo lilifanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara mjini Musoma, na kuhudhuriwa na viongozi wa mashirika mbalimbali, viongozi wa Serikali kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa, Brigedia Jenerali Evans Mtambi.
Rhobi amesema mashirika mengi yanakabiliwa na changamoto za kifedha katika kutekeleza miradi, hivyo yana wajibu wa kubuni vyanzo vya mapato vya ndani ili yaweze kuendelea kuhudumia jamii. Kwani wafadhili wengi wa nje kwa sasa wamesitisha au kupunguza misaada kwa mataifa yanayoendelea.
Pia ameyaomba mashirika hayo kushirikiana kwa pamoja na kujenga ubia madhubuti na Serikali, taasisi za kifedha, wadau wa maendeleo pamoja na wananchi ili kufikia malengo tarajiwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Mtambi, aliyekuwa mgeni rasmi katika jukwaa hilo, ameyataka mashirika hayo kuwa na mipango inayoendana na mipango ya Serikali ili kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Pia ameyahimiza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, kuzingatia sheria za nchi, na kuhakikisha fedha wanazopata kutoka kwa wafadhili zinawafikia walengwa ipasavyo.
Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Patrick Mafuru, ameyataka mashirika hayo kuzingatia sheria, ikiwemo kufanya kazi kwa kuzingatia usajili, kulipa ada ya mwaka kwa wakati, kutoa taarifa za utekelezaji kwa wakati, na kushirikiana na Serikali katika maeneo ambako miradi inatekelezwa.







