Na Ghati Msamba
Musoma: Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Agnes Methew Marwa, ametoa msaada wa mifuko 20 ya saruji, tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 500 pamoja na vifaa vya michezo katika Shule ya Msingi Azimio iliyopo mjini Musoma.
Msaada huo umetolewa katika viwanja vya shule hiyo wakati wa mahafali ya 68 ya wahitimu wa Darasa la Saba mwaka 2026, ambapo Agnes alikuwa mgeni rasmi.
Akizungumza katika mahafali hayo, Agnes aliwahimiza wahitimu kutokata tamaa katika safari yao ya elimu, akisisitiza kuwa kuhitimu elimu ya msingi si mwisho wa masomo, bali ni hatua ya kuendelea na elimu ya juu zaidi.
Alisema yuko tayari kuwasaidia wanafunzi watakaofanya vizuri na kuendelea na kidato cha kwanza kwa kuwapatia baadhi ya mahitaji ya shule kupitia taasisi yake ya Agnes Foundation.
“Nawahimiza msikate tamaa. Kuhitimu shule ya msingi si mwisho wa elimu. Endeleeni kusoma kwa bidii na kuitangaza vizuri Shule ya Msingi Azimio,” alisema Agnes.
Aidha, Agnes alieleza kuwa juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuboresha elimu nchini, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, zinapaswa kuungwa mkono na wadau mbalimbali.
“Kwa juhudi zake Rais Samia Suluhu Hassan za kuipaisha elimu kwa watoto wetu, nipo tayari kumuunga mkono kwa asilimia 90,” alisema.
Katika hatua nyingine, aliwahimiza wazazi kushirikiana kwa karibu na walimu katika kuhakikisha watoto wanalelewa na kusoma katika mazingira bora yatakayowawezesha kufanya vizuri katika masomo yao.
Pia aliwataka walimu kuendelea kujituma katika kutekeleza majukumu yao ili kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi shuleni hapo.
Katika mahafali hayo, Mbunge Agnes pia alikabidhi vyeti kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika maeneo mbalimbali ya shughuli za maendeleo ya shule, akiwapongeza kwa juhudi zao na kuwataka kuendelea kuwa mfano bora kwa wanafunzi wengine.


