SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana imewasihi vijana kote nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa yanayoanza Agosti 11, 2026 mkoani Dodoma, huku ikisisitiza kuwa tofauti za kimazingira hazipaswi kuwa kikwazo cha vijana kufikia ndoto zao za kiuchumi na kijamii.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Bi. Jenifa Omolo, amesema maadhimisho hayo ya siku mbili yatakayofanyika kuanzia Agosti 11 hadi 12, 2026 katika Ukumbi wa Uriyo, Njia Panda ya Nzuguni, yanalenga kuwakutanisha vijana zaidi ya 1,000 ili kujadili hatima na fursa zao za maendeleo ikiwa ni moja ya agenda kuu za utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.
“Mwaka huu, maadhimisho hayo yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: "Different Contexts, Common Aspirations" (Mazingira Tofauti, Fursa Sawa kwa Vijana)”. Bi. Omolo amebainisha kuwa kaulimbiu hiyo inatambua ukweli kwamba ingawa vijana wanaishi katika mazingira yanayotofautiana — iwe vijijini au mijini, wenye elimu rasmi au ujuzi wa mtaani—wote wana matarajio yanayofanana ya kupata elimu, ajira, mitaji na maisha yenye staha.
Mambo yatakayojadiliwa kwenye Maadhimisho hayo, kuanzia Tarehe 11 Agosti: Kongamano maalum litakalojadili ajira, afya ya vijana, Akili Unde (AI), na uzalendo, litakalofunguliwa na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Bi. Susan Ngongi Namondo. Tarehe 12 Agosti: Kilele cha maadhimisho hayo ambapo maazimio ya vijana yatawasilishwa rasmi, huku Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nanauka, akihutubia taifa kama Mgeni Rasmi.
Aidha, Waandishi wa Habari na Wadau wanatarajia kuona utekelezaji wa vitendo zaidi utakaogusa changamoto za ajira zinazowakabili mamilioni ya vijana nchini. "Mazingira yanaweza kuwa tofauti, lakini matarajio ya vijana ni ya pamoja na kila kijana anastahili fursa ya kusonga mbele."
✍️wizara ya vijana


