Na Emmanuel Chibasa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara imewanoa waandishi wa habari mkoani humo kuhusu majukumu yao katika kuzuia na kupambana na rushwa pamoja na umuhimu wa kutoa taarifa sahihi kwa umma.
Mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika leo 27 Agosti 2026 katika ofisi za TAKUKURU Mkoa wa Mara, yakilenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari ambao ni miongoni mwa wadau muhimu katika kutoa elimu kwa jamii na kuibua mianya ya rushwa.
Akifungua mafunzo hayo, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mara, Sadiki Nombo, amesema taasisi hiyo imekuwa na utaratibu wa kutoa semina na mafunzo kwa wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari ili kuwaongezea uelewa kuhusu majukumu ya TAKUKURU na nafasi yao katika mapambano dhidi ya rushwa.
Nombo amesema moja ya majukumu ya TAKUKURU ni kutoa elimu kwa umma, hivyo waandishi wa habari wana nafasi kubwa ya kuwafikia wananchi na kuwaelimisha kuhusu madhara ya rushwa pamoja na umuhimu wa kutoa taarifa wanapobaini viashiria vya vitendo hivyo.
Amesema TAKUKURU pia inafuatilia matumizi mabaya ya ofisi za serikali kwa maslahi binafsi, kuchunguza tuhuma za rushwa, kufuatilia matumizi ya fedha za umma pamoja na kufanya uchambuzi wa mifumo ili kubaini na kuzuia mianya inayoweza kuchochea rushwa.
“Mbali na kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya rushwa, tunafuatilia matumizi mabaya ya ofisi za serikali kwa matumizi binafsi, kuchunguza tuhuma za rushwa, ufuatiliaji wa fedha za umma pamoja na uchambuzi wa mifumo,” amesema Nombo.
Amewataka waandishi wa habari pamoja na jamii kwa ujumla kutoa taarifa kuhusu mianya ya rushwa katika maeneo yao, ikiwemo matumizi mabaya ya rasilimali za umma na fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wake, Afisa Habari na Mawasiliano wa TAKUKURU Mkoa wa Mara, Agnes Karatibu, amewataka wananchi kufuatilia vipindi na taarifa zinazotolewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari ili kupata elimu kuhusu masuala ya rushwa na kutumia fursa hizo kutoa taarifa kuhusu kero zenye viashiria vya rushwa katika maeneo yao.
Naye Eunice Kiwia akizungumza wakati akitoa mada, ametoa wito kwa wananchi kuepuka kutoa hongo wanapohitaji kupata huduma, huku akiwataka kuzingatia taratibu rasmi za malipo na utoaji wa zawadi ili kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuchukuliwa kuwa rushwa.
TAKUKURU inaendelea kutekeleza jukumu lake la kuzuia na kupambana na rushwa kwa kushirikisha jamii na wadau mbalimbali, huku ikisisitiza kauli mbiu yake: “Kuzuia rushwa ni jukumu lako na langu, tutimize wajibu wetu.”















