Serikali na TARI Waokoa Wahanga 160 Matukio ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu

0


 Na AngelaSebastian, 

Bukoba : Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Tanzania Relief Initiative (TARI) pamoja na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi imefanikiwa kuwaokoa jumla ya wahanga 160 wa usafirishaji haramu wa binadamu katika kipindi cha Julai 2025 hadi Februari 2026.

Kati ya wahanga hao, 126 waliokolewa ndani ya mipaka ya Tanzania, huku 34 wakiokolewa kutoka nje ya nchi, hatua inayodhihirisha kuimarika kwa ushirikiano wa kitaifa na kimataifa katika kupambana na uhalifu huo.

Takwimu hizo zimetolewa na Afisa kutoka Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Joseph, wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wasimamizi wa sheria mkoani Kagera.

Mafunzo hayo yamewakutanisha askari wa Polisi, Maafisa Uhamiaji, Waendesha Mashtaka wa Serikali na Mahakimu, yakilenga kuwaongezea uelewa wa namna ya kutambua, kuchunguza na kushughulikia kesi za usafirishaji haramu wa binadamu kwa ufanisi zaidi.

Joseph alisema Serikali imeelekeza nguvu zake katika maeneo manne muhimu ili kuhakikisha Watanzania pamoja na watu wote waliopo nchini wanakuwa salama dhidi ya mtandao wa usafirishaji haramu wa binadamu.

Alitaja maeneo hayo kuwa ni kuzuia uhalifu huo kupitia utoaji wa elimu kwa jamii, kuimarisha mfumo wa sheria, kuwalinda na kuwaokoa wahanga pamoja na kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua za kisheria kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali, sekta binafsi na nchi washirika.

"Serikali imejipanga kuhakikisha hakuna Mtanzania anayejihusisha na usafirishaji haramu wa binadamu. Tunafanya hivyo kwa kutoa elimu, kuimarisha sheria, kuwaokoa na kuwalinda wahanga, kuwafikisha wahusika mahakamani na kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi," alisema Joseph.

Alifafanua kuwa Sheria ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu (The Anti-Trafficking in Persons Act Na. 6 ya mwaka 2008) imefanyiwa maboresho mara kadhaa, huku marekebisho ya hivi karibuni yakifanyika mwaka 2026 ili kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu huo.

Kwa mujibu wa Joseph, sheria hiyo inaweka adhabu kali kwa watakaobainika kujihusisha na usafirishaji haramu wa binadamu, ikiwemo faini ya kati ya Shilingi milioni 50 hadi milioni 300, kifungo cha hadi miaka 30 jela au adhabu zote mbili kwa pamoja, kutegemeana na uzito wa kosa.

Alisisitiza kuwa mafanikio ya mapambano hayo yanategemea ushirikiano wa wananchi, vyombo vya dola na wadau mbalimbali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tanzania Relief Initiative (TARI), Edwin Mugambila, alisema mafunzo hayo yamelenga kuboresha uwezo wa wasimamizi wa sheria ili kuongeza ubora wa uchunguzi, ukusanyaji wa ushahidi na uendeshaji wa mashauri mahakamani.

Alisema takwimu zinaonyesha kuwa baadhi ya kesi zimekuwa zikiharibika kutokana na mapungufu katika upelelezi na ukusanyaji wa ushahidi, jambo linalowanyima haki wahanga wa uhalifu huo.

"Tunatarajia kuona maboresho makubwa kuanzia hatua za uchunguzi, upelelezi, ukusanyaji wa ushahidi hadi kesi zinapofikishwa mahakamani. Tukifanya kazi kwa weledi, wahalifu watawajibishwa kwa mujibu wa sheria na wahanga watapata haki yao," alisema Mugambila.

Alibainisha kuwa kwa Tanzania Bara, Mkoa wa Kagera unashika nafasi ya pili baada ya Morogoro miongoni mwa mikoa 10 inayoongoza kwa matukio ya usafirishaji haramu wa binadamu.

Mikoa mingine iliyotajwa ni Iringa, Dar es Salaam, Mwanza, Tabora, Geita, Shinyanga, Mara na Kilimanjaro.

Alieleza kuwa Kagera ni mkoa wa kimkakati kutokana na mipaka yake na nchi kadhaa za Afrika Mashariki, hali inayoufanya kuwa njia mojawapo inayotumiwa na mitandao ya usafirishaji haramu wa binadamu.

Mugambila amesema watoto wa kike na wanawake ndio waathirika wakubwa wa biashara hiyo haramu, huku maeneo ya vijijini na mipakani yakiongoza kwa matukio mengi.

Ameeleza kuwa mara nyingi wahanga hutoka katika familia zenye kipato cha chini na hurubuniwa kwa ahadi za ajira zenye mishahara mikubwa, elimu au maisha bora.

Baada ya kukubali safari hizo, baadhi yao huishia kulazimishwa kufanya kazi za ndani bila malipo stahiki, biashara ya ngono, kuombaomba au kazi nyingine za kinyonyaji huku wakinyang'anywa nyaraka zao za kusafiria, simu na kuzuiwa kuwasiliana na familia zao.

Katika matukio mengine, alisema wahanga hukumbana na vitisho, unyanyasaji na hata biashara haramu ya viungo vya binadamu.

Mugambila aliwataka wananchi kuwa makini wanapoona watu wanaowafuata watoto au vijana kwa ahadi za kazi bila kufuata taratibu za Serikali.

Aliwashauri kutoa taarifa mapema kwa vyombo vya dola au kupiga simu ya bure 195 ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kupata ushauri na msaada.

"Ushirikiano wa wananchi ni silaha muhimu katika kukomesha biashara hii haramu. Taarifa zinazotolewa mapema zinaweza kuokoa maisha ya watu wengi na kuwafikisha wahalifu mbele ya sheria," amesema.

Wakili wa Serikali na Mwendesha Mashtaka Kiongozi Mkoa wa Kagera, Amani Kyando, amesema mafunzo hayo yataongeza uwezo wa waendesha mashtaka katika kushughulikia kesi za usafirishaji haramu wa binadamu na kuwasaidia wahanga kutoa ushahidi unaokubalika mahakamani.

Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia, Wanawake na Watoto wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera, Mkaguzi wa Polisi Suzan Kamwaga, amesema polisi ndio hupokea taarifa nyingi za awali kutoka kwa wahanga, hivyo mafunzo hayo yatawawezesha kuandaa majalada ya uchunguzi kwa weledi na kuondoa mianya inayoweza kuhatarisha kesi mahakamani.

Amesema wahanga wengi wanaokutana nao ni watoto wa kike, wafanyakazi wa ndani na watu wanaoingia au kuishi nchini bila vibali halali.









Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top