Na Emmanuel Chibasa
Ni jambo la kawaida kuona madereva wa pikipiki
maarufu kama bodaboda pamoja na vyombo vingine vya usafiri Musoma na maeneo
mengine nchini, wakibeba na kusafirisha mitungi ya gesi ya kupikia yenye gesi kutoka
kwa watoa huduma na kupelekwa majumbani ikiwa imelazwa.
Hali hii watu wengi wanaweza
kuona ni jambo la kawaida kwa kuwa ni
njia rahisi y kwa wateja au watoa huduma kuwafikishia wateja huduma kwa haraka
lakini pengine hawana elimu ya madhara na hatari inayoweza kujitokeza.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma
za Nishati na Maji (EWURA) Inatoa
tahadhari kuwa tabia hiyo, inaweza kuwa chanzo cha ajali kubwa ya moto na hata
milipuko inayoweza kugharimu maisha ya watu.
Sio jambo geni kuona dereva
wa boda boda au baiskeli anaondoka kwenye duka la gesi au barabarani akiwa
amefunga mtungi mkubwa wa gesi upande wa nyuma wa pikipiki au baiskeli yake,
Mtungi huo umelazwa kwa usawa huku akipita katikati ya magari, waenda kwa miguu
na wafanyabiashara wa pembezoni mwa barabara.
.Kwa Nini Mitungi Haipaswi Kulazwa?
Mamlaka ya Udhibiti huduma za
Nishati na Maji Kanda ya Ziwa(EWURA), wanaeleza
kuwa mitungi ya gesi ya LPG imeundwa kubebwa na kusafirishwa ikiwa imesimama
wima na sio kulazwa kama baadhi ya watu wanavyofanya.
Mhandisi
Nyirabu Musira ni Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa anasema sababu ya kusafirisha
mitungi hiyo ya gesi ikiwa imesimama ,ni kwamba ndani ya mtungi kuna gesi na
kimiminika (liquefied petroleum gas). Mtungi unapolazwa na kusafirishwa kutoka sehemu moja kwenda
nyingine kimiminika hicho kinaweza
kufika kwenye sehemu ya valve au regulator na kuongeza hatari ya uvujaji wa
gesi.
Anasema
wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari kwa kusafirisha gesi ikiwa imesimama ili
kuepusha uharibifu wa Valve na iwapo uvujaji huo utatokea karibu na moto,
sigara, mfumo wa umeme au cheche yoyote unaweza kusababisha mlipuko au moto
mkubwa.
‘Unapokua unatumia gesi
hakikisha eneo gesi ilipo kuna hewa ya kutosha na madirisha yako wazi, na
endapo utahisi harufu ya gesi ujue gesi yako inavuja hivyo unatakiwa uchukue
tahadhari kubwa kwa mfano utakiwi kuwasha moto au kuwasha na kuzima swichi ya
umeme kukiwa na hali hiyo, sababu swichi ya umeme unapowasha au kuzima wakati
gesi inavuja inaweza kusababisha mlipuko” Amesema Nyirabu



