Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe wakati akifunga maadhimisho
ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2026 kama Mgeni Rasmi, ametembelea banda
la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kupongeza kasi ya utoaji
wa huduma huku akitoa maagizo mazito kuhusu matumizi ya mifumo ya kidijitali.
Akiwa
kwenye banda hilo, Waziri Shemdoe amewaelekeza wataalamu na watendaji wa sekta
ya ardhi kuongeza muda wa kutoa huduma hadi tarehe 30 mwezi huu ili kuhakikisha
wananchi wote wanaozunguka kupata huduma wanatuliwa kero zao kabla ya kufunga
rasmi kliniki hizo za ardhi.
“Sasa
maelekezo yangu hawa wa ardhi wabaki hapa mpaka tarehe 30 ili hawa wote
wanaozungujka hapa waje wapewe huduma” alisema Waziri Prof. Riziki Shemdoe
Katika
hatua nyingine Waziri huyo amewataka wataalamu wa Ardhi nchini kuendelea kutumia
mifumo ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi hasa katika mchakato wa
kufuatilia hati.
"Mimi
leo nimekuwa mgeni rasmi wa kufunga Wiki ya Utumishi, ninawaelekeza: mahali
popote ambapo mifumo inatakiwa itumiwe, itumiwe mifumo," alisisitiza Waziri
Shemdoe huku akibainisha kuwa changamoto kubwa iliyopo nchini kwa sasa ni
masuala ya ardhi, na uwepo wa kliniki hizo unaleta faraja na tabasamu kwa
wananchi.
Kwa
upande wake, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dodoma Bw. Geofrey
Mwamusojo ameeleza kuwa hadi sasa banda hilo limefanikiwa kuwahudumia wananchi
1,306 waliokuwa na mahitaji mbalimbali, ikiwemo ushauri wa kisheria na utatuzi
wa migogoro. Kati yao, wananchi 310 wamefanikiwa kukabidhiwa hati zao za miliki
papo hapo.
Nao
wananchi waliopata fursa ya kupata hati zao kwa haraka wamepongeza juhudi hizo,
wakieleza kufurahishwa kwao na weledi wa watendaji wa sekta ya ardhi.
"Nimefurahi
sana kupata hati katika siku ya leo. Sijachukua muda mrefu, nimeanza mchakato
kama majuzi na leo nimefanikiwa kuipata," alisema Robert Michael
Naye
Bi. Kibibi Shaban aliongeza kwa kuwasihi wananchi wenzake kuwa wavumilivu na
kuhakikisha wanarasimisha maeneo yao, hususan wanaponunua viwanja vipya ili
kuwa na usalama wa miliki zao.


